MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa sehemu ya kuonesha njia katika utendaji kazi wake jambo ambalo linatakiwa kuigwa na wafanyakazi wengine.
Amesema Rais amekuwa kiongozi wa mfano, kwa kutafuta ufumbuzi wa changamoto za wananchi kitu ambacho kinatakiwa kufanywa na wafanyakazi wengine, kwa kufanya kazi kwa weledi na kutaondoa kero kwenye jamii.
Kunenge amesema kwa kipindi cha miaka mitano, mkoa huo umepokea Sh. trilion 1.53 fedha za miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali
Akizungumzia suala la uwekezaji wa viwanda, amesema mkoa huo, unaongoza hapa nchini kuwa na viwanda zaidi ya 1,500 huku ajira zikiendelea kuongezeka.
Kunenge pia amesema, kwa sasa wameanza mazungumzo na wawekezaji wa mkoa huo, ili waweze kutoa mikataba ya ajira, kwa wafanyakazi sambamba na kuchangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Wakati huo huo, Kunenge ametoa wiki moja kwa kila taasisi iliyoguswa kutoa majibu ya changamoto za wafanyakazi zilizoelezwa kwenye risala ya wafanyakazi.
“Sekta binafsi na za umma mjibange kufanya kazi wa bidii na kuongeza mapato zingatieni katika kushinda kama ilivyo kwa Rais asivyoamini kwenye kushindwa.”
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Pwani, Ramadhan Kinyogori, amemshukuru Rais kwa kuendelea kutatua changamoto za wafanyakazi.
Awali akisoma risala ya wafanyakazi Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Pwani, Susan Shesha, amepongeza serikali kwa kuwa sikivu na kuanza kutekeleza ufanyaji wa mabaraza katika wilaya zote za mkoa wa Pwani, huku watumishi wakipatiwa huduma bora mahala pa kazi.
Shesha alibainisha changamoto ambazo wafanyakazi wanahitaji zishughulikiwe kuwa ni pamoja na mishahara ya watumishi, ambayo haiendani na hali halisi ya maisha ya sasa.
Mratibu huyo amesema vyama vya wafanyakazi wa Mkoa huo, vimeomba waajiri kutimiza wajibu wao sambamba na kuongeza kasi ya ulipaji wa madeni kuepuka migogoro.
Mmoja wa wafanyakazi waliopata zawadi ya mfanyakazi bora, Nasra Mondwe, ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata ‘R’ nne za Rais Samia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED