Polisi waendelea uchunguzi mauaji ya Mbunge Charles Ong'ondo Were

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 AM May 02 2025
Polisi waendelea uchunguzi mauaji ya Mbunge Charles Ong'ondo Were
Picha: Mtandao
Polisi waendelea uchunguzi mauaji ya Mbunge Charles Ong'ondo Were

Maafisa wa Polisi jijini Nairobi kutoka Idara ya Makosa ya Jinai wanaendelea na uchunguzi kubaini waliohusika na mauaji ya Mbunge wa Kasipul, Charles Ong'ondo Were, ambaye alipigwa risasi na kuuawa jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya polisi, tukio hilo linaonesha kuwa lilipangwa kwa umakini na kutekelezwa kwa usahihi mkubwa.

Tukio hilo liliripotiwa kutokea saa moja na nusu usiku karibu na mzunguko wa Makaburi ya City, kando ya barabara ya Ngong. Gari jeupe aina ya Toyota Crown, ambalo liliripotiwa kumchukua Mbunge Were pamoja na watu wengine wawili, lilikuwa limesimama kwenye taa nyekundu wakati pikipiki iliyokuwa na watu wawili ilisogea na kusimama kando yake.

Kwa mujibu wa mashuhuda, abiria aliyekuwa kwenye pikipiki hiyo alishuka na kumfuata Were aliyekuwa ameketi ndani ya gari hilo, kisha akafyatua risasi upande wake. Baada ya kumpiga risasi, mshambuliaji huyo alikimbia haraka na kupanda tena pikipiki hiyo ambayo iliondoka kwa kasi na kutoweka.

Polisi wamesema uchunguzi bado unaendelea, huku wakiwataka wananchi wenye taarifa zozote muhimu kuhusu tukio hilo kujitokeza kusaidia katika kuwatambua na kuwanasa wahusika.