SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Shinyanga, limeiomba serikali kufanya marekebisho ya kikokoto na kurudisha cha awali cha asilimia 50.
Mratibu wa TUCTA mkoani Shinyanga, Ramadhani Pangara, amebainisha hayo leo Mei Mosi, 2025, wakati akisoma risala ya wafanyakazi mkoani humo, kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.
"Tatizo la kikokotoo linatunyima usingizi, tunaomba serikali ilirudishe cha zamani cha asilimia 50 na siyo cha sasa kinatuumiza," amesema Pangara.
Nyingine ni waajiri wa sekta binafsi kutozingatia sheria na taratibu za ajira na hata kutowapatia wafanyakazi wao mikataba ya kazi.
Alitaja nyingine, ni baadhi ya waajiri kutoruhusu wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi, na wanaotaka hupatiwa vitisho na hata wengine kufukuzwa kazi.
Waliulalamikia pia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kupunguza baadhi ya vifufurushi na kwamba ni kuwanyanyasa watumishi.
Pia, walilalamikia tatizo la baadhi ya waajiri, kutowapatia motisha wafanyakazi wao na hata kuwanyima zawadi katika Mei Mosi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi, wakati serikali ikiendelea kushughulikia changamoto ambazo zinawakabili.
Amesema serikali ilishatoa ajira mpya, watumishi kupandishwa madaraja na kwamba itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Amesema kwa changamoto ambazo zimewasilishwa zote watazifanyia kazi, huku akimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Salum Hamduni, kuunda timu ambayo watashirikiana na vyama vya wafanyakazi, ili kuitatua changamoto moja baada ya nyingine.
Katika hatua nyingine, amewataka wananchi pamoja na wafanyakazi, kwamba wajitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, ambalo tayari limeshaanza mkoani humo na litadumu kwa siku saba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED