WADAU wa zao la mpunga nchini, wametakiwa kuzichangamkia fursa zipatikanazo kwenye mnyororo wa thamani kwenye zao la mpunga.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dk. Hussein Mohamed Omar, amesema hayo wakati akifunga Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa Zao la Mpunga, uliofanyika jijini Dodoma.
Dk. Omar amesema kuwa kutokana na fursa lukuki kwenye zao hilo, wananchi wa sehemu mbalimbali linapolimwa, wameinuka kimaisha kutokana na mauzo ya zao hilo.
Pia Dk. Omar amebainisha kuwa zao la mpunga ni zao la pili linalokua kwa kasi nchini, huku uzalishaji wake ukiongezeka kwa asilimia tano.
Amebainisha kuwa tija ya zao hilo, inatarajiwa kuongezeka kutoka tani mbili kwa hekta, hadi kufikia tani 4.4 katika kilimo cha mvua na tani 7.34 kwa hekta kwenye umwagiliaji.
Pia Dk. Omar ameishukuru serikali kupandisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, kutoka shilingi bilioni 294.16 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia shilingi trilioni 1.249 mwaka 2024/2025.
Amesema, ongezeko hilo linachangia kuongezeka kwa tija katika uzalishaji wa zao la mpunga.
Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji katika Mkoa wa Morogoro, Dk. Rozalia Rwegasira, ameshauri wakulima wa zao la mpunga, kutumia zaidi kilimo cha umwagiliaji, ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao hilo.
Pia, ameshauri watumie mbegu bora, zenye kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ili kuongeza zaidi tija na uzalishaji.
Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji katika Mkoa wa Tabora, Abrahaman Mndeme, amesema lengo la serikali ni kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka tani milioni nne za sasa na kufikia tani milioni saba, ifikapo 2030.
Mwakilishi wa Kampuni ya Japan International Cooperation Agency (JICA) Tanzania, Ara Hitoshi, amesema ushindani kwenye uzalishaji wa zao la mpunga unaongezeka na mkutano wa wadau wa zao hilo, utasaidia kufanikisha azma ya serikali kukuza zao la mpunga.
Mkutano huo wenye Kauli mbiu isemayo ‘Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo na Matokeo chanya ya Tasnia ya Mpunga’, umehudhuriwa na wakurugenzi wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara.
Pia, makatibu tawala uchumi na uzalishaji wa mikoa ya Mbeya, Shinyanga, Katavi, Tabora na Morogoro, Wasindikaji na wakulima kutoka maeneo yanayozalisha kwa wingi zao la mpunga hapa nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED