Padri Kitima atuma salamu akiwa hospitalini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:09 PM May 01 2025
Padri Kitima atuma salamu akiwa hospitalini
Picha: Mtandao
Padri Kitima atuma salamu akiwa hospitalini

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema amemtembelea hospitalini Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, na kumfikishia ujumbe wa watanzania wapenda haki.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mwabukusi ameandika:

 "Nimemtembelea Father Dr. Charles Kitima. Hakika lilikuwa shambulio baya lenye lengo la kudhulumu maisha."

Ameongeza kuwa hali ya Padri Kitima inaendelea vizuri, na kwamba Mungu ni mwema. Aidha, ametoa ujumbe alioueleza kuwa umetoka kwa Padri Kitima mwenyewe kwa ajili ya watanzania wote. Ujumbe huo unasema:

  1. Lazima tuwe imara kusimamia masuala ya msingi katika Taifa.
  2. Hatutakiwi kuogopa kulipa gharama katika kusimamia haki na wajibu wetu kwa Taifa.
  3. Kila mmoja atalipa gharama kwa kiasi chake, na hilo lazima tuwe tayari.
  4. Tunapozungumzia mambo ya msingi kitaifa yanayotakiwa kurekebishwa ili uchaguzi ufanyike kwa haki, tusiogope kulipa gharama.

Padri Kitima alishambuliwa Aprili 30, 2025, majira ya saa nne usiku, mara baada ya kutoka katika eneo alilokuwa akipata kinywaji. Alipokuwa akielekea maliwatoni, alishambuliwa kwa kupigwa na kitu butu kichwani.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ya Mei 1, 2025, imeeleza kuwa mtu mmoja anashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na shambulio hilo dhidi ya Padri Kitima.