‘Wagombea wasifanywe kitega uchumi cha kanisa’ Askofu Nkwande

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 03:55 PM Apr 18 2025

Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza Mhashamu Askofu Renatus Nkwande.
Picha; Mpigapicha Wetu
Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza Mhashamu Askofu Renatus Nkwande.

Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza Mhashamu Askofu Renatus Nkwande amewaonya mapadri wa kanisa hilo kutotumia fursa ya uchaguzi na kuwatesa wanaotarajia kugombea uongozi katika ngazi mbalimbali kwa kuwatwisha mizigo ya michango ya fedha kwa kigezo cha kuwa wanahitaji kuchaguliwa.

Askofu Nkwande amesema kumekuwa na desturi kikifika kipindi cha uchaguzi, waumini wenye nia ya kuwania nyadhifa mbalimbali kutumika kama sehemu ya ujenzi wa makanisa na nyumba za mapadri kutokana na kuwa wanahitaji kuungwa mkono.

Amesema kufanya hivyo ni kuwatesa na kuwatwisha mizigo isiyostahili kwani wanapoitwa wanashindwa kukataa na kuahidi fedha nyingi ambazo ni nje ya uwezo wao ili kujionesha kwa waumini.

“Huwa ninafurahi nikikuta amealikwa muumini wa kawaida kama mgeni rasmi katika harambee lakini siyo hawa kwani mnawatesa na hawawezi kukataa mwishoe unasikia anahidi kutoa Sh.milioni 500 wakati fedha hiyo hata hana,” amesema Askofu Nkwande.

“Mwaka huu una uchaguzi, mapadre mnaweza kutumia uchaguzi huu kama fursa….fursa ya kupata pesa ili tujenge makanisa yetu, tujenge nyumba za mapadre na tukachangiwa kwele bila kujua hata hizo pesa zinatoka wapi,” 


“Tuna najisi makanisa yetu, nyumba tutakazokuwa tunalala kwa uroho wa pesa. Kanisa haitatokea hata siku moja likajitosheleza au likawa tajiri tuzipende hizi pesa za waumini wetu ndogo ndogo hizi tunazogombana nao ndizo zinatakatifuza makao na makanisa yetu,” alisema Askofu Mkuu Nkwande.