Mwana Fa akagua Uwanja Benjamini Mkapa

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 04:23 PM Apr 29 2025
Mwana Fa wa pili kushioto akikagua Uwanja Benjamini Mkapa
Picha: Shufaa Lyimo
Mwana Fa wa pili kushioto akikagua Uwanja Benjamini Mkapa

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana Fa, amesema ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa utachukua muda wa wiki mbili pekee.

Amesema lengo ni kuhakikisha Tanzania inaandika historia kwa kuandaa fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Barani  Afrika.

Simba, itaanza ugenini mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya RS Barken katika Fainali itakayopigwa Mei 17, 2025, nchini Morocco.

Mei 25, mwaka huu, itakuwa dimba la nyumbani katika  mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, inatarajiwa kuwa tukio la kihistoria, kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali ya mashindano  ya kimataifa.

Akizungumza leo, Aprili 29, 2025, alipofanya ukaguzi wa uwanja huo, Dar es Salaam, Mwinjuma amesema serikali imejipanga kuhakikisha fainali hiyo inachezwa katika mazingira bora, huku akibainisha kuwa kazi ya ukarabati tayari imeanza.

Mwana Fa akikagua Uwanja Benjamini Mkapa
Ameongeza kuwa kuna maelekezo ambayo wamepeana yakiwamo ya saa 24 na 48, kuhakikisha yanatekelezwa kwa muda na wakati uliopangwa.

“Tumeagiza matrekta kutoka Zanzibar na Tanga, tayari yanawasili na kazi inaanza mara moja. Inawezekana kukamilisha kabla ya muda uliopangwa, no benchi za kukalia,” amesema Mwinjuma.

Ameongeza kuwa ukarabati huo, unahusisha maeneo mbalimbali ikiwamo uwekaji wa viti vipya zaidi ya 30,000 tayari vimefungwa, huku wakitarajia kuziba uwazi kwa ajili ya mchezo huo.

Amefafanua kuwa eneo lingine ni pamoja na  ukarabati wa chumba cha udhibiti wa matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni na tayari viwanja vya mazoezi, Meja Jenerali Isamuhyo na Mo Arena  kwa ajili ya timu, vimekidhi na vipo tayari.

“Tunataka mpaka CAF wakija kukagua wakute kila kitu kiko tayari. Lengo ni kuhakikisha ifikapo Mei 25, 2025, fainali inachezwa hapa nyumbani,” amesema.

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, ameipongeza serikali kwa juhudi kubwa wanazofanya kuhakikisha fainali hiyo inafanyika Tanzania. 

Amesema Simba inajiandaa kikamilifu kupeperusha vyema bendera ya taifa.

“Tunaendelea na maandalizi, tuna michezo mitano ya Ligi kabla ya kuelekea fainali, hivyo  tunataka kuleta furaha kwa watanzania kwa kupata matokeo mazuri,” amesema Mangungu.

Amewapongeza watanzania waishio Afrika Kusini, kwa kuonesha umoja wao, bila kujali timu zao kwa kujitokeza katika mchezo wa nusu fainali na kuomba watanzania hapa nchini kuiga mfano wa kujitokeza katika mchezo huo.