Viongozi CHADEMA Kibiti wajiuzulu, watangaza kuhama chama

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:06 PM May 20 2025
Viongozi CHADEMA Kibiti wajiuzulu, watangaza kuhama chama
Picha:Mtandao
Viongozi CHADEMA Kibiti wajiuzulu, watangaza kuhama chama

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Kibiti, Mohamed Seif, pamoja na viongozi wengine watatu wa chama hicho, wametangaza kujiuzulu nyadhifa zao na kujiondoa rasmi CHADEMA, wakipinga kile walichokiita ukosefu wa haki na ushiriki wa kweli wa kisiasa.

Viongozi hao wametoa tamko hilo leo Mei 20, wakiongozana na Ismail Mpili, mtia nia wa kugombea Ubunge wa Jimbo la Kibiti katika Uchaguzi Mkuu ujao. Wamesema uamuzi wao umetokana na chama kushindwa kusaini kanuni za uchaguzi, hali iliyokifanya kujitoa katika uchaguzi wa Oktoba 2025, jambo walilolielezea kama usaliti kwa wanachama na demokrasia.

"Tumelazimika kuchukua uamuzi huu mgumu kwa sababu hatuwezi kubaki katika chama ambacho hakilindi haki za msingi za wanachama wake, hususan uhuru wa kutoa maoni na kushiriki katika uchaguzi," amesema Mohamed Seif.

Kwa upande wake, Ismail Mpili alisema kuwa alijiandaa kwa ajili ya kugombea ubunge Kibiti, lakini kitendo cha chama kushindwa kusaini kanuni hizo kinamnyima haki ya kidemokrasia ya kushiriki katika mchakato wa uchaguzi.

"Hili ni jambo la msingi ambalo linahitaji kusemewa ili lifanyiwe marekebisho. Siwezi kuendelea kuwa sehemu ya mfumo unaoninyima haki yangu ya kugombea," alisema Mpili.

Viongozi hao wameeleza kuwa wataendelea na harakati zao za kisiasa kupitia jukwaa jingine, na wametangaza kuwa kesho Mei 21, wataeleza rasmi chama kipya watakachojiunga nacho.