Serikali yataja sababu kuzuia Wakenya kusikiliza kesi ya Lissu

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 05:02 PM May 20 2025
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro
Picha: Mtandao
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu hatua ya kuwazuia raia kadhaa wa Kenya waliowasili nchini hivi karibuni kwa lengo la kufuatilia kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ikisema walikiuka sheria kwa kuingia bila kuwa na leseni ya kufanya shughuli za uwakili nchini.

Akizungumza leo Mei 20, jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara ya Katiba na Sheria katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, ameeleza kuwa wageni hao walikuwa wanavunja sheria za nchi kwa kuingia kama wanasheria bila kibali halali.

“Jana, Mheshimiwa Rais alizungumzia suala hili kwa ustarabu mkubwa. Lakini sisi wengine ustarabu siku nyingine huwa tunaacha nyumbani. Wapo ndugu zetu kutoka Kenya walizuiliwa kwenye Uwanja wa Ndege wakidai wamekuja kushiriki katika kesi ya Tundu Lissu kwa ajili ya kutetea haki za binadamu,” amesema Dk. Ndumbaro.

Amefafanua kuwa watu hao hawakuwa na leseni ya kufanya shughuli za uwakili nchini Tanzania, jambo ambalo linapingana na sheria za nchi.

“Mimi ni mwanasheria, na kwa uelewa wangu wa kitaaluma, watu hao hawakuwa na leseni ya kufanya kazi ya uwakili hapa. Hivyo, walichokuja kufanya ni uvunjifu wa sheria. Mbaya zaidi, huko kwao wameshindwa kushughulikia matatizo yao, lakini wanataka kuingilia ya kwetu – hiyo ni aina ya unafiki,” amesema kwa msisitizo.

Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa Tanzania inazingatia na kulinda haki za binadamu kwa kiwango cha juu, hivyo haina haja ya watu kutoka nje kuja kutoa somo.

“Watanzania hatutaki unafiki katika eneo la haki za binadamu. Kama taifa, tupo vizuri katika hilo, na ninaunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais,” ameongeza.