Kenya yajitenga na Martha Karua kuzuiwa kuingia Tanzania

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:37 PM May 20 2025

Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura.
Picha: Mtandao
Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura.

Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura amesema Tanzania imetenda kwa mujibu wa haki yake ya uhuru kwa kuwazuia watu kadhaa wa kisiasa na wanaharakati wa Kenya, wakiongozwa na Martha Karua na kwamba Kenya haikuwa na jukumu katika uamuzi huo.

Mwaura ameyasema hayo leo wakati akijibu kuhusu hatua ya kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu, Martha Karua, aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, na wanaharakati wengine wanne kuzuiwa kuingia Tanzania juzi.

Inaelezwa kuwa Mather na wenzake walitaka kuingia nchini kwa lengo la kwenda kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu ambayo inaendelea kusikilizwa kwatika mahakama ya kisutu mkoani Dar es Salaam.

“Ikiwa serikali ya moja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaamua kumkataa mtu binafsi kuingia nchini mwao, ina mamlaka ya kufanya hivyo,” Mwaura amesema.


Amesisitiza kuwa serikali ya Kenya inaheshimu uhuru wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na haiingilii maamuzi yao ya ndani.

“Ikiwa wameamua hivyo, huo ni uamuzi wao. Hatujui kwa nini watamzuia mtu, na serikali ya Kenya haihusiki,” amesema.


Siku ya Jumapili, Mather na wengine wawili walifukuzwa nchini Tanzania, wakati Mutunga, pamoja na wanaharakati wa haki Hussein Khalid na Hanifa Adan, walizuiliwa walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

BBC