Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya jambo kubwa katika mikoa ya Kaskazini kupitia Filamu ya The Royal Tour, iliyochagiza ukuaji wa sekta ya utalii, kuongezeka kwa mapato na wananchi kunufaika kiuchumi.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla, ameyasema hayo leo Juni 4,2025, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara yake mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Makalla amesema watalii wanapoingia nchini mapato huongezeka na kuchangia kuwapo kwa mzunguko wa fedha.
Amesema hayo yote yanatokana na ubunifu wa Rais Samia aliyeona umuhimu wa kuitangaza Tanzania kupitia filamu hiyo ambayo wananufaika.
“Katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, mapato ya utalii yameongezeka na nyie Manyara mnafaidika, mko karibu na Karatu, Tarangire na Mbuga ya Manyara,” amesema Makalla.
Amesisitiza kuwa kupitia filamu hiyo sekta ya utalii imeimarika, imesaidia kuutangaza utalii ulioko nchini katika mataifa mbalimbali na kuongeza mapato nchini yatokanayo na utalii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED