Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam wameziomba taasisi za kifedha kuhakikisha zinawawezesha kupata huduma za fedha za kigeni, wakisema kuwa huduma hiyo ni muhimu kwa uendeshaji wa biashara zao zinazowahusisha wateja wa ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa Julai 5, 2025, na Mwenyekiti wa Soko la Kariakoo, Severini Mushi, wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki ya Ecobank lililofunguliwa rasmi ndani ya eneo la soko hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mushi alisema kuwa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni ni hitaji la msingi kwa wafanyabiashara na wateja kutoka mataifa mbalimbali wanaofika Kariakoo kwa shughuli za kibiashara.
“Kariakoo ni kitovu cha biashara nchini. Huduma za kifedha zenye urahisi, usalama na ufanisi zitawawezesha wafanyabiashara wetu kukua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema Mushi.
Aidha, alilishukuru benki ya Ecobank kwa kufungua tawi karibu na jamii ya wafanyabiashara, akibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza mzunguko wa fedha na kurahisisha miamala ya kibiashara kwa haraka na ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ecobank Tanzania, Dk. Charles Asiedu, alisema benki hiyo imejikita katika kutoa huduma bora zinazozingatia ukuaji wa teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili bandia (Artificial Intelligence) ili kuwahudumia wateja kwa ubunifu zaidi.
“Tuna mtandao mpana wa huduma katika zaidi ya nchi 33 barani Afrika. Uwepo wa tawi letu hapa Kariakoo ni fursa ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa hapa na wenzao wa mataifa mengine,” alisema Dk. Asiedu.
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Shukuruni Mkondya, alisisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kuwa karibu na maeneo ya kibiashara, akieleza kuwa hatua hiyo huongeza fursa za kuunganishwa na huduma za kidijitali na hivyo kuchochea ukuaji wa biashara, hususan kwa wanawake wafanyabiashara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED