Bhutan, nchi yenye wananchi 700,000 isiyowahi kutawaliwa

By Enock Charles , Nipashe
Published at 02:52 PM Jun 06 2025
Bhutan.
Picha:Mtandao
Bhutan.

Bhutan ni nchi ndogo iliyopo katika bara la Asia, ikipakana na India upande wa kusini na China upande wa kaskazini. Ina idadi ya watu wapatao 700,000 na eneo la takribani kilomita za mraba 38,394.

Dini kuu inayoongoza nchini humo ni Ubuddha, ambayo chimbuko lake ni India tangu enzi za maisha ya Buddha. Ubuddha umeenea sana Bhutan na umejikita katika maisha ya kila siku ya watu wake, ikiwa ni pamoja na utamaduni, siasa na elimu.

Tofauti na nchi nyingi za Asia, Bhutan haikuwahi kutawaliwa na wakoloni, ingawa iliingia katika uhusiano wa karibu na Milki ya Uingereza. Kupitia Mkataba wa Punakha wa mwaka 1910, Bhutan ilikubali kupokea ushauri wa Waingereza katika masuala ya sera ya kigeni, lakini iliendelea kuwa huru katika mambo ya ndani.

Baada ya Uhuru wa India mwaka 1947, uhusiano huo uliendelezwa kupitia mkataba mpya wa mwaka 1949 uliotiwa saini huko Darjeeling, ambapo India na Bhutan walikubaliana kuheshimu uhuru wa kila upande.

Bhutan iliingia rasmi katika Umoja wa Mataifa mwaka 1971 na kwa sasa ina uhusiano wa kidiplomasia na zaidi ya nchi 56 duniani. Ingawa inategemea jeshi la India kwa ulinzi wa mipaka yake ya nje, Bhutan ina vitengo vyake vya kijeshi vya ndani kwa ajili ya usalama wa ndani.

Mnamo mwaka 2008, nchi hiyo ilipitisha katiba mpya iliyoanzisha mfumo wa serikali ya bunge, ikiwa na Bunge la Kitaifa lililochaguliwa na wananchi pamoja na Baraza la Kitaifa kama chombo cha ushauri.

Bhutan inajivunia kuwa taifa linalolinda utamaduni wake, mazingira, na falsafa ya "Furaha ya Taifa Zima" (Gross National Happiness) badala ya kuangazia tu pato la taifa kama kipimo cha maendeleo.