MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mtambani iliyoko Bunju mkoani Dar es Salam Venance Mwasamakwela, amesema shule hiyo inaupungufu wa madawati 285 na hivyo kufanya wanafunzi wengine kukosa sehemu ya kukaa wakati wa masomo.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2002 hadi sasa ina wanafunzi 2,606 ina madawati 580 kati ya 865 yanayo hitajika. Masamakwela aliyasema hayo jana shuleni kwake katika hafla ya kupokea msaada wa madawati 65 kutoka kwa Kampuni ya Ulinzi Gardaword kwa ajili ya kusaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokosa nafasi ya kukaa.
Alisema msaada huo, utasaidia kupunguza idadi ya watoto 195 waliokuwa wanakosa nafasi huku akiwataka wadau wengine kuwaunga mkono katika upungufu uliobakia. “Tunashukuru kwa msaada huu wa madawati tutayatunza ili wanufaike wanafunzi wengi zaidi tunaomba pia na wadau wengine wajitokeze kutuunga mkono” alisema mwalimu huyo.
Mkurugenzi wa Gardaword, Goodluck Lukumani alisema anaamini mchango wao utaleta mabadiliko chanya katika shule hiyo, na kufanya wanafunzi kusoma kwa uhuru akisisitiza samani za darasani zina mchango mkubwa kumfanya mwanafunzi afaulu mitihani yake.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Elimu Msingi Manispaa ya Kinondoni, Chitegese Dominic alisema madawati hayo yatapunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hiyo.
“Itasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi kitaaluma kutokana na wao kupata nafasi za kusoma na kuandika kwa uhuru.Katika Manispaa ya Kinondoni, kuna upungu wa madawati katika shule nyingi vyumba vya walimu, matundu ya vyoo, na mahitaji mengine ya kitaaluma tunaomba wadau na serikali waendele kutusaida kutatua changamoto hizo” alisema Dominic
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED