Wanafunzi 214,141 wachaguliwa Kidato cha 5 na Vyuo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:18 PM Jun 06 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.
Picha:Mtandao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.

Wanafunzi 214,141 wamekidhi vigezo na sifa za msingi za kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi, ualimu na afya kwa mwaka 2025.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameyasema hayo jijini Dodoma  wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu uchaguzi wa wanafunzi hao.

Amefafanua wanafunzi hao ni waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2024 ambao walipata daraja la I-III.


“Kati ya wanafunzi hao 149,818 sawa na asilimia 69.96 wakiwemo wasichana 76,491 na wavulana 73,327 wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule 694 za sekondari za Serikali, wanafunzi 2,875 wakiwamo wasichana 1,057 na wavulana 1,818 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vinne vya elimu ya ufundi,”amesema.


Kadhalika, amesema wanafunzi 2,214 wamechaguliwa kujiunga vyuo vya afya ngazi ya Stashahada, 1,609 vyuo vya ualimu na 57,625 vyuo vya kada mbalimbali.