Mkazi wa Gongo la Mboto matatani kusababisha ajali gari la CHADEMA

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 01:52 PM Jun 06 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama.

Mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, Yahaya Bakari Idd (43), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, ajali hiyo ilitokea Juni 5, 2025 katika eneo la Mataa ya Tumbaku, Kata ya Mafisa, Manispaa ya Morogoro.

Gari alilokuwa akiendesha Yahaya, aina ya Ford Ranger lenye namba T.661 DQL, mali ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), liliacha njia na kugonga lori aina ya Scania lenye namba T.340 DWW / T.976 CJE ambalo lilikuwa limeegeshwa katika kisima cha mafuta.

Kamanda Mkama amesema kuwa abiria watatu waliokuwa ndani ya gari la Ford Ranger walipata majeraha madogo, walipatiwa matibabu na tayari wameruhusiwa kurudi nyumbani.

KIFO CHA FUNDI UJENZI CHAZUA MASWALI

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linaendelea na uchunguzi wa kifo cha fundi ujenzi asiye na makazi maalum, Odilo Anania Sumi (80), ambaye mabaki ya mwili wake yalikutwa katika makaburi ya Kola, Manispaa ya Morogoro.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkama, mabaki hayo yaligunduliwa Juni 5, 2025, na uchunguzi wa awali umeonesha kuwa marehemu alikuwa akiishi mitaani.

Kwenye eneo la tukio, Polisi walikuta sehemu ya mavazi ya marehemu, dawa na karatasi yenye namba za simu ya mkononi, ambavyo vinaendelea kufanyiwa uchunguzi kwa ajili ya kusaidia kubaini mazingira ya kifo chake.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio yote mawili na limewataka wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kufanikisha upelelezi.