Rais Samia ataja sifa za watumishi wa Mungu

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:39 PM Jun 05 2025
Rais Samia Suluhu Hassan, akiongozana na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.
Picha:Mpigapicha Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan, akiongozana na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.

Rais Samia Suluhu Hassan, ametaja mambo yanayowatambulisha watumishi wa kweli wa Mungu, akisema ni kuwajali wenye mahitaji katika jamii.

Amesema watumishi wasiofanya hivyo, wanatumikia usherani na mambo yanayofanana na hayo.

Rais Samia ameyasema hayo Dar es Salaam leo Juni 05, 2025 alipokuwa kwenye hafla ya kuchangia harambee ya ujenzi wa kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu, kinachojengwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

“Mnachofanya huu ndio utumishi wa dini...kuwajali wenye mahitaji. Kuisaidia jamii. Sote tunawiwa kushiriki na kuwajali wenye mahitaji maalumu. Kwa kazi hii muhimu mliyoianzisha, mmeonesha kutekeleza mafunzo ya maisha na matendo ya miujiza ya Yesu Kristo.

“Hamjaishia tu kuwaonesha matendo ya huruma, mmesimama kuwatetea na kuwawezesha wenye mahitaji maalumu waishi maisha bora. Kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwakarimu wageni, kuwavika wasio na nguo na kuwatembelea wagonjwa ni jukumu letu sote.

Katibu Mkuu ametaja mambo kadhaa ambayo kanisa hili linafanya…ndugu zangu huu ndio utumishi wa dini. Kazi hii mnayofanya, inapeleka ujumbe kwa wale waliojionesha kama watumishi wa dini, lakini kwa kweli ni watumishi wa ushetani ama mambo mengine.

Huu ndio ujumbe muhimu kwao. Utumishi wa dini ndio huu, kuwajali wenye mahitaji, kufanya mambo mbalimbali ya kijamii, kuisaidia jamii, kujenga jamii iliyobora,” amesema.