Waajiri wasisitizwa kutumia mtandao kuwasilisha madai ya fidia WCF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:32 AM Jun 06 2025
Dk. Abdulsalaam Omar ni Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF alifungua kikao kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu.

Kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi WCF Julai 1, 2025, WCF imetoa Mafunzo kwa Wadau wa Mfuko huo ya usalama na afya mahala pa kazi na kutoa elimu kuhusiana na uwasilishaji wa madai ya fidia kwa njia ya mtandao.

Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Dar es Salaam yakiwa yamewalenga Watumishi kutoka Sekta binafsi na ile ya Umma.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini- WCF, Dk. Abdulsalaam Omar amesema wanatumia nafasi hiyo pia kuwaelimisha wadau shughuli mbalimbali ambazo zinafanywa na WCF ikiwemo mafao ya fidia kwa wafanyakazi yanayotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).


‘‘Katika siku hii tuna wadau mbalimbali ambao ni wawakilishi wa waajiri wakiwemo maafisa Rasilimali watu, Maafisa usalama na Afya Mahala Pa kazi na tunakutana nao hapa kwaajili ya kubadilishana mawazo, kukumbushana namna ya kubaini vihatarishi katika maeneo yao ya kazi lakini pale ambapo ajali au magonjwa yanapokuwa yanatokea ni namna gani ya kuweza kuwasilisha madai mapema, lakini pia tunataka kupeana uelewa wa namna ya kuweza kufanya uchunguzi wa ajali zinazotokana na kazi na namna bora ya kuweza kudhibiti hizo ajali’’ amesisitiza Dk. Omar

Kwa upande wa washiriki, Hamid Shebuge, Meneja kutoka kiwanda cha sukari Bagamoyo, amezungumza mara baada ya kushiriki mafunzo hayo na kusema WCF imewaletea program ya Vision Zero ambayo inalenga kutoa Elimu kwa Watu, Wafanyakazi, na Menejimenti, kila mtu anatambua wajibu wake katika kuhakikisha anaokoa na kulinda usalama wa watu na miundo mbinu.

‘‘Kwahiyo kupitia program hii na sisi tumepatiwa elimu kiwandani kwetu kwani tulipata mafunzo ambayo tunaendelea kufanyia kazi. Miaka 10 ya WCF sisi tunashukuru mfuko huu kuendelea kutufikia na kutuhudumia” ameongeza Shebuge


Naye George Alando kutoka DSM Corridor Group amesema mafunzo hayo yamesisitiza umuhimu wa matumizi ya Tehama wakati wa kuwasilisha madai ya fidia kwa wafanyakazi, pale ambapo wanapata ajali, pamoja na kujifunza sheria inayoongoza WCF ikiwemo masuala ya Usalama Mahala Pa Kazi vilevile namna gani wao kama Waajiri na Waajiriwa waweze kuzingatia na kuwaelimisha wafanyakazi wenzao.


Jill Kaijage kutoka TIPER amesema: 

‘‘Mafunzo haya yameweza kutusaidia sisi kama Waajiri kujifunza Sheria zinazosimamiwa na WCF na kubaini changamoto zilizopo endapo mwajiri anakuwa hajatoa michango kwa wakati na pindi mfanyakazi anapokuwa amefikwa madhila, na kufahamu taratibu zinazofuatwa na WCF. Vilevile, pale ambapo Mwajiri anakuwa hajatoa taarifa ya Wafanyakazi waliopo katika Taasisi yake na Sheria zinazotakiwa kuchukua mkondo’’ amesema.


Julieth Joseph kutoka Ensol Tanzania Limited, amesema katika mafunzo hayo amejifunza mambo mengi ikiwemo msisitizo wa kujitahidi kuzuia mapema zaidi kuliko kusubiri ajali ama matukio mengine kama magonjwa kutokea “na nimependa zaidi namna ambavyo WCF wanajitahidi kutumia njia ya mtandao kurahisisha uwasilishaji wa taarifa ambao pia unasaidia utunzaji wa Kumbukumbu’ amesema. 

WCF imeendesha mafunzo hayo ikiwa na lengo la kuendelea kuwapa uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko huo, Usalama na Afya Mahala Pa Kazi, Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi na Hatua za kufuata wakati wa kuwasilisha Madai ya Fidia kwa Wafanyakazi hususani kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao.