Mwanaharakati wa Haki za Wanawake, Emma Nyerere, amesema kuwa kuyumba kwa amani ni ishara ya kusambaratika kwa umoja wa kitaifa, hivyo kila Mtanzania ana jukumu la kuhakikisha jamii haiingii kwenye mgawanyiko, matabaka, wala ubaguzi wa aina yoyote.
Akizungumza leo, Juni 5, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa kumbukizi ya kifo cha Imam Khomein iliyofanyika katika Kituo cha Utamaduni wa Iran nchini, Nyerere alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani iliyopo, akieleza kuwa ikipotea, gharama ya kuirejesha ni kubwa mno.
"Tunakumbushwa kuwa ni lazima kulinda amani na umoja wetu. Mambo makubwa hufanyika kwa umoja, na amani tuliyonayo tunatakiwa kuitunza kwa gharama yoyote," amesema Nyerere.
Ameongeza kuwa jamii inapaswa kuendelea kuwa na mshikamano, kuepuka kujiona bora, ubaguzi wa kidini, kikabila au kijinsia, na kutambua kuwa palipo na umoja ndipo haki hupatikana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni wa Iran nchini, Dk. Mohsen Maarefi, ametoa rai kwa vijana kuenzi na kuendeleza urithi wa amani uliosimikwa na viongozi wa kihistoria kama Imam Khomein na Mwalimu Julius Nyerere.
“Maadhimisho haya ni jukwaa muhimu la kutafakari na kuenzi mchango mkubwa wa viongozi hawa wawili waliopigania haki, umoja na amani duniani. Vijana ndiyo nguzo kuu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kitaifa," amesema Dk. Maarefi.
Naye Balozi wa Amani, Joseph Simba, amewahimiza vijana kutambua nafasi yao kama viongozi wa sasa, si kesho, na hivyo kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani.
"Vijana wasikubali kutumiwa kuvuruga amani. Chuo hiki cha Utamaduni wa Iran kinawalea vijana katika misingi ya amani na kuwaandaa kuwa mabalozi wa kweli wa utulivu na mshikamano. Bila amani, hakuna elimu, hakuna maendeleo," amesema Simba.
Kumbukizi hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, vijana kutoka taasisi mbalimbali za elimu, pamoja na wadau wa masuala ya amani na utamaduni, ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wa Imam Khomein katika kuhimiza maadili ya kijamii, utu na mshikamano wa kimataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED