Kwa umbali wa takribani kilomita 100 kutoka Mikocheni jijini Dar es Salaam hadi Mtaa wa Misweduka, Kata ya Bwawa, Wilaya ya Kibaha katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Kampuni ya The Guardian Limited imefika kwa lengo la kuwapatia wanafunzi wa kike 208 taulo za kike zitakazowasaidia kujistiri wanapokuwa kwenye hedhi.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo katika kurudisha kwa jamii, baada ya kushinda tuzo ya Gazeti Mahiri kupitia tuzo za Samia Kalamu Awards. The Guardian Limited, inayochapisha magazeti ya Nipashe kwa Kiswahili na The Guardian kwa Kiingereza, imetoa jumla ya pakiti 1,000 za taulo za kike kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mbali na msaada huo, kampuni hiyo pia imeendesha huduma ya upimaji wa ugonjwa wa selimundu kwa vijana ambao hawajaoa wala kuingia kwenye mahusiano ya kudumu, kwa lengo la kuwasaidia kutambua hali zao kiafya mapema.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi taulo hizo, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Beatrice Bandawe amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuwashukuru wasomaji na jamii kwa ujumla ambao wamekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya kampuni hiyo.
"Tunatambua kuwa kati ya asilimia 30 hadi 40 ya wanafunzi wa kike hukosa masomo kila mwaka kutokana na ukosefu wa taulo za kike. Hili ni tatizo kubwa ambalo linaathiri maendeleo ya kielimu kwa mtoto wa kike. Kama chombo cha habari tunacho wajibu siyo tu wa kuhabarisha bali pia kuchangia ustawi wa jamii yetu," amesema Bandawe.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Moses Magogwa, ameipongeza The Guardian Limited kwa hatua hiyo, akisema kuwa si tu wameandika habari, bali wametekeleza kwa vitendo kwa kurejesha fadhila kwa jamii.
"Kwa kutoa taulo hizi mmewapunguzia changamoto kubwa wasichana hawa. Sasa watasoma kwa amani na kujiamini, bila kuhofia kukosa masomo wakati wa hedhi. Hili ni somo kubwa kwa sisi sote kwamba tukibarikiwa, tusiisahau jamii inayotuzunguka," amesema Magogwa.
Naye Mkuu wa Shule ya Mbwawa Misweduka, Getrude Amory, ameishukuru kampuni hiyo kwa jitihada zao, hasa ikizingatiwa kuwa wamevuka umbali mrefu hadi kufika shuleni hapo kwa ajili ya wanafunzi.
"Msaada huu utawatia moyo wanafunzi wetu wa kike, utaongeza morali katika masomo yao na kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo yao ya kitaaluma," amesema Amory.
Tukio hilo ni sehemu ya mfululizo wa matukio ya kurudisha kwa jamii yanayoandaliwa na The Guardian Limited, yakiwemo ya kupanda miti katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED