Duvii aandaa mashindano ya Samia Cup kuinua vipaji Mkinga

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 07:26 PM Jun 04 2025
Duvii aandaa mashindano ya Samia Cup kuinua vipaji Mkinga
Picha:Mpigapicha Wetu
Duvii aandaa mashindano ya Samia Cup kuinua vipaji Mkinga

Imeelezwa kuwa michezo ni ajira muhimu kwa vijana, kwa kuwa huwatoa katika makundi hatarishi na kuwawezesha kutambua nafasi na wajibu wao katika jamii, huku wakiwa na fursa ya kuonekana katika timu kubwa kitaifa na kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Makampuni ya Duvii Farms na Duvii Transport, Saidi Rashid Duvii, wakati wa fainali ya Kombe la Samia Cup Mkinga zilizofanyika katika Wilaya ya Mkinga. Katika fainali hizo, timu ya Chafupozi iliibuka bingwa kwa kuifunga Kasera kwa mikwaju ya penalti 2 kwa 1.

Duvii, ambaye ni mdau mkubwa wa maendeleo ya michezo, alisema mashindano hayo yameandaliwa kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya michezo, huku pia yakilenga kurudisha fadhila kwa wananchi wa wilaya hiyo kupitia makampuni yake.

“Tumeanzisha ligi hii kwa sababu asilimia kubwa ya vijana wako mtaani. Kwa kufanya hivi, vijana wataweza kuonekana, kupata ajira na hata kujiajiri. Kuna vipaji vingi vinaishia mashambani, hivyo mashindano haya ni njia ya kuwaonesha watu kwamba vipaji hivyo vipo,” alisema Duvii.

Aidha, alibainisha kuwa mashindano hayo yatakuwa endelevu, yakilenga kuwaleta vijana pamoja, kujenga umoja na mshikamano miongoni mwao.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union ya jijini Tanga, Ahmed Aurora, alisema lengo la mashindano hayo ni pamoja na kusaka vipaji, na kusaidia kuanzishwa kwa timu ya kudumu ya wilaya ya Mkinga.

“Kupitia mashindano haya, tunakwenda kutengeneza timu moja bora kabisa, ambayo itashiriki ligi kuanzia ngazi ya chini hadi juu. Tayari vipaji vimeshaonekana,” alisema Aurora.

Katika mashindano hayo:

  • 🏆🥇💵Mshindi wa kwanza alizawadiwa kombe, shilingi milioni 5 taslimu, na medali.


  • 🥇💵Mshindi wa pili alipokea shilingi milioni 3 na medali.


  • 💵Mshindi wa tatu alizawadiwa shilingi milioni 2.


  • 💵Mshindi wa nne alipata shilingi milioni 1.