Selimundu janga nchini

By Sanula Athanas , Nipashe
Published at 11:15 AM Jun 04 2025
Selimundu janga nchini
Picha: Nipashe Digital
Selimundu janga nchini

Ugonjwa selimundu sasa ni janga nchini. Serikali imekiri asilimia 15 ya wananchi wamebeba vinasaba vya selimundu, huku 34,220 wakiendelea na matibabu ya maradhi hayo.

Katika hotuba yake bungeni jijini Dodoma juzi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka 2025/26, Waziri Jenista Mhagama alibainisha Tanzania ni miongoni mwa nchi tano duniani zinazoongoza kwa idadi kubwa wagonjwa wa selimundu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Nigeria inaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na selimundu ikifuatwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), India, Tanzania na Uganda.

Waziri Jenista aliarifu Bunge juzi kuwa hivi sasa asilimia 15 ya Watanzania wanaishi na vinasaba vya ugonjwa huo. 

Tovuti rasmi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jana saa 09:05 alasiri ilionesha Tanzania mwaka huu inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 68,153,004.

Kwa kuzingatia takwimu za Wizara ya Afya kwamba asilimia 15 ya wananchi wanaishi na vinasaba vya selimundu, ina maana kuwa watu 10,222,950 (milioni 10.2) wanaishi na vinasaba vya maradhi hayo nchini.

"Wizara imeendelea na upimaji wa ugonjwa wa selimundu kwa watoto wachanga. Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya watoto wachanga 3,171 walipimwa vinasaba vya ugonjwa wa selimundu ili kubaini ugonjwa katika hatua za awali.

Takwimu kuhusu Sikoseli.

 "Hadi sasa jumla ya wagonjwa 34,220 wa selimundu wanaendelea kupatiwa matibabu. Zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa hawa wanapata matibabu kwa kutumia dawa ya Hydroxyurea na wagonjwa 11 wa Selimundu walipandikizwa uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH)," alisema.

Katika kudhibiti ugonjwa huo, Waziri Jenista alisema wizara kwa kushirikiana na wadau imeanzisha kampeni maalumu ya elimu ya selimundu na kampeni ya vunja mduara ambayo inalenga vijana kutambua hali zao ya vinasaba. 

"Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya vijana 10,601 kutoka katika mikoa ya Mwanza, Morogoro, Pwani, Mara, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Tabora walipatiwa elimu na fursa ya kupima vinasaba vya ugonjwa wa selimundu. 

"Wizara pia ilitoa elimu ya ugonjwa adimu wa himofilia kwa wazazi, walezi na wagonjwa 1,690 katika Mikoa ya Morogoro, Manyara, Tanga na Arusha," Waziri Jenista alisema.

Alisema kupanuka kwa huduma za himofilia na selimundu kutapunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyotokana na magonjwa hayo.

KUHUSU SELIMUNDU

Desemba 31 mwaka jana, Nipashe ilichapisha ripoti maalumu kuhusu selimundu, ikiangazia namna ugonjwa unavyotesa kimwili, kiuchumi na kijamii.

Kuna safari zisizoisha hospitalini, kulala wodini, mahitaji ya kuongezwa damu mara kwa mara, huku upande wa pili ukiakisi gharama kwa anayemhudumia mgonjwa.

Kuna cha simanzi zaidi, serikali inakiri nusu ya wanaozaliwa na selimundu hufariki dunia ndani ya miaka mitano ya kuzaliwa kwao. Zaidi ya watoto 14,000 huzaliwa na maradhi hayo nchini kila mwaka. Kati yao, zaidi ya 10,000 huzaliwa mikoa ya Kanda ya Ziwa. Mwanza pekee huzaliwa zaidi ya watoto 1,700 kila mwaka wenye tatizo hilo. 

Wataalamu wa selimundu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando jijini Mwanza na Hospitali ya Rufani ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma walizungumza kwa kina na Nipashe kuhusu ugonjwa huu.

Walisema kutibu selimundu ni kupandikiza uloto. Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, gharama ya matibabu hayo nchini inaanzia Sh. milioni 50 hadi 55 kwa kila mgonjwa. Upandikizaji uloto nchini kwa sasa unafanywa BMH kwa kugharamiwa na Mfuko wa Rais.

Kwa watoto 14,000 wanaozaliwa na tatizo hili, maana yake serikali italazimika kutenga zaidi ya Sh. bilioni 770 kwa ajili ya matibabu ya watoto hao kila mwaka.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto na Mtaalamu wa Selimundu katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, Emmanuela Ambrose anashauri watu wenye vinasaba vya ugonjwa huo wasioane.

"Matibabu ya selimundu ni ghali, hususani katika kupandikiza uloto. Hivyo, ili kuepuka haya, lazima jamii ikubaliane kupima kabla ya ndoa ili kuwaepusha watoto wetu na maumivu wanayopitia watoto wenzao wenye maradhi ya selimundu," bingwa huyo anashauri.

Bingwa wa Maradhi ya Watoto MNH, Dk. Evance Godrey, anatoa fasili ya kitaalamu kuhusu selimundu, akiutaja ni ugonjwa wa kuzaliwa nao kutokana na kuurithi kutoka kwa wazazi kupitia vinasaba.

Anasema ni tatizo la muda mrefu katika seli nyekundu za damu ambako husababisha baadhi ya seli nyekundu za damu kuwa na umbo lisilo la kawaida. Badala ya kuwa na umbo linalofanana na diski, zinakuwa na umbo kama la nusu mwezi (mwezi mwandamo).

"Umbo la nusu mwezi la seli nyekundu za damu ni kwa sababu zinajumuisha umbo lisilo la kawaida la hemoglobini. Hemoglobini ni dutu iliyo katika seli nyekundu za damu ambayo inabeba oksijeni. Umbo la nusu mwezi linasababisha seli nyekundu za damu kuvunjika kwa urahisi na zisitoshee vizuri katika mishipa midogo ya damu ili kusafirisha oksijeni.

 "Seli nyekundu za damu zisizo za kawaida hazipiti katika mishipa midogo ya damu kwa urahisi, hivyo viungo vya mwili havipati damu ya kutosha. Mtiririko wa damu unapozuiwa, mtu hupata maumivu makali kwenye viungo na wakati mwingine jeraha kwenye maungio ya nyonga.

"Dalili hatari zaidi za selimundu ni pamoja na kiharusi (kupooza), moyo kutanuka, moyo kushindwa kufanya kazi, figo kushindwa kufanya kazi, upungufu wa damu, maumivu makali ya kifua, uume kuvimba, vidonda sugu vya ngozi na bandama kusinyaa.

"Dalili zingine ni manjano kwenye macho au ngozi na mtoto kuchelewa kukua (udumavu). Mara nyingi dalili za selimundu hujitokeza mtoto anapotimiza umri wa miezi sita hadi minane tangu kuzaliwa kwake," Bingwa Godfrey anafafanua.