Makalla ataja makubwa ya Samia, Sumaye akoleza, anayeona kasoro ana matatizo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 06:43 PM Jun 04 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo  CCM, Amos Makalla.
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla, ametaja makubwa yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, akisema amerudisha utulivu, amani na tumaini kwa Watanzania lililokuwa limepotea na kusisitiza anayeona kasoro ana matatizo.

Sumaye, amesema Rais Samia amefanya kazi kubwa kurudisha uhusiano wa kimataifa na kufanya sasa wanaheshimika duniani.

Amesema alipochukua nchi alitangaza kuwa hataki kuhusishwa na dhuluma ambapo watu walionyanganywa mali zao akazirudisha, akaunti zilizofungwa wakati ni fedha halali nazo akarudisha.

Pia, amesema Rais Samia ametekeleza miradi mikubwa mbalimbali na watu wanafungua biashara hakuna anayedhulumiwa, kunyanganywa fedha benki, amerudisha utulivu, amani na tumaini kwa Watanzania.

Sumaye ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani Manyara, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya siku saba ya Mwenezi CCM inayohusisha mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

Akihutubia mkutano huo, Makalla amesema Sumaye ameeleza kwa kirefu juu ya mambo makubwa yaliyofanywa chini ya Rais Samia, akieleza walikotoka, walipo sasa na mwelekeo wa miaka mingi inayokuja ambapo msingi wake unaendelea kuwekwa na Rais Samia.

“Sina haja kueleza miradi mingi iliyofanywa,  ninaamini wananchi walipokwenda katika uchaguzi yupo aliyefurahia umeme, aliyefurahia amani, aliyefurahia kujengwa josho la ng’ombe, aliyefurahia kituo cha afya, aliyefurahia zahanati au maji,” amesema.

Makalla amesisitiza kuwa mambo haliyofanywa ni mengi, akitolea mfano mikoa ya Kaskazini, akieleza jambo kubwa lililofanywa ni kukuza utalii kupitia filamu ya Royal Tour iliyochezwa na Rais Samia.

“Imefanya kazi kubwa mikoa Manyara, Arusha na Kilimanjaro mapato ya utalii yameongezeka na nyie Manyara mnafaidika nayo.

“Mko karibu na Karatu mbuga ya Manyara Tarangile nyie ni wanufaika, watalii wanapokuja mzunguko wa fedha unaongezeka yote ni jitihada za Rais Samia mzalendo anayekuja na ubunifu aliyekwenda kucheza filamu kuitangaza Tanzania, leo tunafaidika,” amesema.