Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla, amesema Mkoa wa Manyara ni ngome ya Chama Cha Mapinduzi.
Amesema wabunge wote mkoani humo ni wa CCM na madiwani watatu waliotokana na upinzani wameanza kurejea chama tawala, amebakia mmoja tu.
Ameyasema hayo leo katika Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani humo, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara, ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya siku saba katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
“Wabunge wote mkoani Manyara ni CCM, kasoro madiwani watatu ambao leo wawili ametangaza hapa kurejea Chama Cha Mapinduzi, amebaki diwani mmoja,” amesema.
Makalla amewaeleza wananchi kuwa mwaka jana alikwenda hapo akiwa na Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwaomba katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijijini kuwachagua wagombea wa CCM.
“Tuliwaambia ngazi muhimu huanzia na vijiji, vitongoji ambao watafanya kazi na madiwani, wabunge na Rais, nasimama kwa heshima kwa niaba ya CCM kuleta shukrani zetu kwa kukipa ushindi wa kishindo wa asilimia 98 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji,” amesema.
Makalla amesema wanafahamu wananchi wanapokwenda kuchagua huangalia mambo mengi ndipo wapige kura, huangalia wamchague nani na chama gani.
Amesema mambo makubwa yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan yamewafanya viongozi mkoani humo wakiwamo wabunge, Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa Wilaya CCM, kuzungumzia Sh. bilioni 700 iliyoshushwa huko kutekeleza miradi ya maendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED