Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Manyara, F.3544 Sajenti Ismail Rashid Katenya (49), amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.
Hukumu hiyo ilisomwa juzi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara, John Kahyoza, katika Wilaya ya Babati.
Katika hukumu hiyo, Jaji Kahyoza alisema mshtakiwa alikiuka Kifungu cha 15 (1)(a), (3)(iii) cha Sheria ya Mwaka 2019 ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Sura ya 95 kama ilivyofanyiwa marejeo.
Kwa mujibu wa Jaji huyo, mshtakiwa pia alikiuka Kifungu cha 18 cha Sheria Namba 5 ya Mwaka 2001, ikisomwa pamoja na Aya ya 23 ya Nyongeza ya Kwanza ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022, pamoja na Vifungu vya 57 (1) na 60 (2)(3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka huo huo.
Aidha, alisema mshtakiwa alikamatwa Januari 22, mwaka 2024 katika Kijiji cha Silaloda, kilichopo Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara.
Jaji Kahyoza alisema mshtakiwa alikamatwa akiwa anasafirisha bunda za mirungi 380 zenye uzito wa kilogramu 160.9, akitumia gari yake aina ya Nissan Patrol yenye namba za usajili T 148 CTB.
Alisema katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 19837 la mwaka 2024, mshtakiwa alinaswa akitoka Arusha. Pia, Jaji alisema upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo saba na mashahidi saba.
Awali, Wakili wa Serikali, Rose Kayumbo, akisaidiana na Wakili Mwandamizi Roberth Kidando, Edith Msenga na Wakili Leonce Bizimana, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani kwa kuwa kosa hilo lina adhabu moja tu.
Wakili Kayumbo aliiomba mahakama itoe amri ya kutaifisha gari lake ambalo lilitumika kusafirisha dawa hizo, ili liwe mali ya serikali.
Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Fides Mwenda, aliyewawakilisha mawakili wa utetezi waliosimamia kesi hiyo—Godfrey Wasonga, Thadey Lister, na marehemu Wakili Joseph Masanja—aliiomba mahakama imuonee huruma na kumpa adhabu ndogo kwa kuwa ni mkosa wa mara ya kwanza, ni mtu mzima na ana wategemezi.
Akitoa utetezi wake, mshtakiwa aliieleza mahakama kuwa alienda shambani kwake Mbulu akiwa amebeba mbegu za vitunguu saumu, lakini baada ya kugongana na gari la Polisi, walimbambikia dawa hizo.
Baada ya utetezi huo, Jaji Kahyoza alimtia hatiani na kumpa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, huku akiamuru gari lake litaifishwe endapo ndani ya siku 60 hakuna mtu yeyote atakayejitokeza kudai kuwa ni mali yake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED