Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kupitia Shule Kuu ya Afya ya Kinywa na Meno, kimepokea msaada wa viti viwili vya kisasa vya kutolea huduma ya afya ya kinywa na meno kutoka Tanzania Cantonese Chamber of Commerce kwa kushirikiana na Foshan DYM Medical.
Viti hivyo vyenye teknolojia ya kisasa vinatarajiwa kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wagonjwa pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kada ya afya ya kinywa na meno.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mkuu wa Shule Kuu ya Afya ya Kinywa na Meno, Dk. Ferdinand Machibya, amesema kuwa viti hivyo vina uwezo wa hali ya juu ikiwemo kamera maalum inayomwezesha mgonjwa kuona hali ya kinywa chake moja kwa moja, jambo linalorahisisha uelewa wa tatizo pamoja na tiba.
“Teknolojia hii inamsaidia daktari kutoa huduma bora kwa wagonjwa wengi kwa wakati mmoja, na pia inarahisisha mafunzo kwa wanafunzi wengi. Hii ni hatua kubwa kwa maendeleo ya taaluma na huduma ya afya ya kinywa na meno hapa nchini,” amesema Dk. Machibya.
Dk. Machibya ameishukuru serikali kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya, na kupongeza wadau waliojitokeza kushirikiana na MUHAS katika kuimarisha mazingira ya utoaji huduma na mafunzo.
“Shule hii ya Kinywa na Meno ni taasisi kubwa nchini inayotoa mafunzo ya taaluma hiyo kuanzia ngazi ya shahada ya kwanza, shahada ya pili hadi ya uzamivu. Tunahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau ili kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi zaidi,” ameongeza.
Ameeleza kuwa kupatikana kwa viti hivyo kutachangia kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi, huku pia vikisaidia katika tafiti mbalimbali zinazofanywa na chuo hicho ili kuongeza maarifa na uwezo wa kitaalamu kwa watoa huduma.
Kwa upande wake, Meneja wa Foshan DYM Medical Instrument Co. Ltd, Bonnie Hong, amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya mchango wao katika kuunga mkono utoaji wa elimu bora na huduma za afya ya kinywa na meno nchini Tanzania.
“Lengo letu ni kusaidia taasisi kama MUHAS kutimiza malengo ya kutoa huduma bora na elimu ya kitaalamu kwa watumishi wa afya, ili hatimaye jamii inanufaika kwa kiwango kikubwa,” amesema Bonnie.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED