Vijana 500 Sumbawanga wajitokeza kumchukulia fomu Aeshi Hilaly

By Mussa Mwangoka , Nipashe
Published at 05:42 PM Jun 04 2025
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly.
Picha:Mtandao
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly.

Wakati baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakikabiliwa na upinzani ndani ya chama hicho, hali ni tofauti kwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly, ambapo vijana zaidi ya 500 wamejitokeza na kudai kuwa watamchukulia fomu ili agombee tena nafasi hiyo.

Wakizungumza leo, Juni 4, 2025, baadhi ya vijana hao ambao miongoni mwao ni wasomi wa vyuo vikuu, makada wa CCM na hata wasiokuwa makada, wamesema nia yao ya kumchukulia fomu Hilaly inatokana na mchango wake mkubwa katika kuhakikisha jimbo hilo linakuwa na maendeleo endelevu.

Mwenyekiti wa mtandao huo ujulikanao kwa jina la Vijana 500, wenye makao yake mjini Sumbawanga, Joseph Ndasi, amesema wamejipanga kuhakikisha wanamchukulia fomu ya ubunge ndani ya CCM pindi zoezi hilo litakapoanza rasmi.

Amesema fedha za kuchukulia fomu hiyo zinatoka mifukoni mwao na tayari zimeandaliwa, huku akieleza kuwa lengo ni kuthamini mchango wa Hilaly katika nyanja mbalimbali za maendeleo, ikiwemo uchumi, jamii na michezo.

“Lengo ni kuhakikisha Aeshi anarudi tena... kuna mambo mengi amefanya katika jimbo hili. Uboreshaji wa miundombinu ya barabara za mitaani, nishati ya uhakika ya umeme, maji, na pia ameongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za afya,” alisema Monica Winston, Katibu wa mtandao huo.

Ameongeza kuwa Hilaly alisimama kidete kuhakikisha sekta ya afya inaboreshwa kwa kiwango kikubwa, kiasi kwamba sasa kila kijiji kina zahanati na kila kata ina kituo cha afya.

“Jamaa amefanikiwa sana... kuna maeneo machache yamebaki, ndiyo tunataka aende akamalizie,” amesisitiza Monica.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dodoma, ambako anahudhuria vikao vya Bunge, Mbunge Aeshi Hilaly amesema ni jambo jema kuona wananchi wanatambua na kuthamini mchango wake wa kimaendeleo katika jamii.

“Nawashukuru kwa kuonyesha upendo wa dhati kwangu. Natambua na kuthamini hicho wanachoenda kukifanya... kimsingi nimefarijika kusikia hivyo, na wamenipa nguvu ya kuja kupambana kwa maslahi mapana ya umma,” amesema mbunge huyo ambaye anapendwa sana na makundi ya wanawake, vijana na wazee.