Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ameipa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela siku saba kuwasilisha mpango kazi wa namna ya kutatua tatizo la uchakavu wa magari 10 ili kuepusha kuathiri utendaji kazi wa halmashauri hiyo.
Agizo hilo limetolewa katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo wa kupokea na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na utekelezaji wake.
Mtanda amesema Halmashauri hiyo inapaswa kuwasilisha mpango huo ndani ya siku saba, mpango ambao utaonyesha matatizo ya magari hayo na gharama za kuyarekebisha. Amesisitiza kuwa baada ya hapo atatoa miezi miwili magari hayo yawe yamekamilika na kuwa katika matumizi, huku akiahidi kuyakagua kwa macho ili kuhakikisha suala hilo halijirudii tena katika vikao vya aina hiyo.
“Utaratibu wangu wa kazi, sitaki kuona magari ya serikali yamepakiwa wakati mengine yanahitaji gharama kidogo sana — mfano milioni moja, mbili au tatu. Hapa Ilemela hamuwezi kushindwa,” amesema.
Aidha, amewataka viongozi wa Halmashauri hiyo kushirikiana na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja na ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuhakikisha wanapata majibu ya hoja nne zilizobainishwa. Pia amesisitiza kwamba hawapaswi kuzalisha hoja mpya bali kuzifunga kwa wakati kwa kushirikisha ipasavyo idara zote zinazohusika.
Akiwasilisha majibu ya ukaguzi huo, CPA Richson Ringo, Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Mkoa wa Mwanza, amesema Manispaa ya Ilemela imepata hati safi (unqualified opinion) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Hata hivyo, amesema baadhi ya hoja hazikufungwa kutokana na kukosekana kwa mikakati thabiti na ya dhati kutoka kwa watekelezaji wa majukumu, pamoja na kutokushirikishwa ipasavyo kwa wakuu wa idara. Sambamba na hilo, baadhi ya majibu ya menejimenti yamekosa vielelezo na ushahidi wa kutosha ili kuwezesha kufungwa kwa hoja hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu, amesema uchakavu wa magari hayo unaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wa halmashauri, hususan katika ufuatiliaji wa mapato na shughuli mbalimbali za nje.
Amesema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa, ikiwemo kuwaita wasimamizi wa magari ili kuandaa mpango kazi utakaobainisha magari yote yenye changamoto.
“Lakini yale magari ambayo tunaona kabisa hatuwezi kuendelea nayo kwa sababu baadhi yake yamechakaa kupita kiasi — hata ukiweka fedha za serikali unakuta baada ya wiki moja gari linaharibika tena — tutajipanga kuyatambua rasmi, kuyatangaza kuwa mali chakavu na kuyaondoa kwa mujibu wa taratibu za kiserikali,” amesema.
Kwa upande mwingine, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga, amesema suala la uchakavu wa magari lilianza tangu Novemba 2012, wakati halmashauri hiyo ilipotenganishwa na Jiji la Mwanza na haikupata magari mapya. Amesema kwa kipindi chote kuanzia mwaka 2015-2020 na 2020-2025, halmashauri imekuwa ikiendelea kununua magari mapya kadri bajeti inavyoruhusu.
Ameeleza kuwa licha ya baadhi ya magari kuwa chakavu, bado halmashauri ina magari zaidi ya 30 yanayofanya kazi, ambapo 10 kati yake yapo katika hali nzuri na mengine yaliyobaki yatafuata utaratibu wa kutangazwa kuwa mali chakavu na kuuzwa.
Mulunga pia amesema kwa kipindi cha takribani miaka mitano sasa Halmashauri ya Ilemela imekuwa ikipata hati safi mfululizo, akifafanua kuwa siri ya mafanikio hayo ni mshikamano uliopo kati ya Baraza la Madiwani, Mkurugenzi, Mbunge na Mkuu wa Wilaya.
“Mkitembea pamoja lazima mtafanikiwa. Ukipata halmashauri ambayo Mbunge anasema peke yake, Mkuu wa Wilaya kivyake, Halmashauri kivyake — huo ni utengano. Ilemela tunashirikiana. Hii ndiyo siri ya mafanikio; hoja za CAG zinakwenda na wakati wake. Mfano leo tumezungumzia taarifa ya mwaka 2023/2024, lakini pia kuna hoja nyingine ambazo utekelezaji wake unaendelea kwa miaka iliyopita kama 2021/2022 na 2022/2023, kila moja ina utaratibu wake,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED