Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, amewataka wanawake kuachana na dhana potofu kuwa hata wasipojitokeza kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan atashinda tu, akisisitiza kuwa suala la uchaguzi si jambo la mzaha.
Makinda ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na mamia ya wanawake wa Mkoa wa Singida katika kongamano lililoandaliwa kwa ajili ya kumpongeza Rais Samia kutokana na maendeleo makubwa aliyoyaleta katika mkoa huo.
“Uchaguzi si mchezo. Kila mtu ana wajibu wa kisheria kuhakikisha anajitokeza kupiga kura. Usiseme ‘mama atapita tu’ — hakuna cha kusema atapita tu,” amesema Makinda.
Ameeleza kuwa mara nyingi wakati wa uchaguzi, baadhi ya watu huonyesha uzembe kwa kudhani kwamba hata wasipoenda kupiga kura, viongozi wanaowataka watashinda tu, jambo ambalo si sahihi.
“Yaani unasema hata nisipopiga kura atapita tu, na wanaosema hivyo mara nyingi ni sisi wanawake. Tunasema Samia ameshapita — sio hivyo, nendeni kapigeni kura,” amesisitiza.
Makinda pia amesema kuwa kwa mujibu wa imani nyingi za dini, kutokupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi ni dhambi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika mchakato huo wa kidemokrasia.
Aidha, amewataka wanawake kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kutokana na mageuzi makubwa aliyoyaleta nchini, hasa katika sekta ya matumizi ya nishati safi kwa wanawake, badala ya kutumia nishati chafu ambayo imekuwa chanzo cha madhara mbalimbali kiafya.
Makinda pia ametoa tahadhari kwa wanawake kutunza vizuri kadi zao za kupigia kura kwa sababu kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu, vitambulisho hivyo huibiwa au kununuliwa na watu wenye maslahi binafsi.
“Nchi hii ndugu zangu, mjiweke vizuri. Hivyo ‘vichinjio’ (kadi za kupigia kura) vinaibiwa, wanaweza kuibiwa hivi hivi mfukoni kwako au wakanunua kwa fedha zao. Vilindeni, mviweke mahali pazuri,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema kuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana, wanawake 900 wa mkoa huo walichukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo uenyekiti wa vijiji, vitongoji na ujumbe wa serikali za vijiji, ambapo kati yao 109 walichaguliwa kuwa viongozi.
Dendego amewahamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa nafasi hizo si za wanaume pekee bali ni kwa Watanzania wote wenye uwezo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeleta maendeleo makubwa mkoani Singida, likiwemo suala la upatikanaji wa umeme ambapo vijiji 441 na vitongoji 1,052 vimefikishiwa huduma hiyo, huku kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji 120 ikiendelea.
“Mkoa wetu umepokea majiko ya gesi ya ruzuku 30,111 ambayo yatauzwa kwa Shilingi 20,800 badala ya Shilingi 48,000. Tutahakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi,” amesema Dendego.
Katika sekta ya afya, Mkuu huyo wa Mkoa amesema zimejengwa zahanati mpya 62, vituo vya afya 22 na hospitali nne za wilaya, huku sekta ya elimu ikiwa imepata shule mpya 12 za msingi, sekondari 40 na shule za amali saba.
Kwa upande wa huduma ya maji safi na salama, Dendego amesema kiwango kimepanda kutoka asilimia 53 hadi kufikia asilimia 86, huku miradi 39 ya maji ikiendelea kutekelezwa na inatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED