Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuvunjwa Juni 23 kupisha Uchaguzi Mkuu

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:30 PM Jun 20 2025
 Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem

Ukomo wa Baraza la Wawakilishi la Kumi (10) Zanzibar unatarajiwa kufikia mwisho Juni 23, 2025, kufuatia hatua ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kulivunja rasmi baraza hilo ili kupisha shughuli za Uchaguzi Mkuu.

Hayo yamesemwa leo Juni 20 na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea kumalizika kwa kipindi cha miaka mitano ya uhai wa baraza hilo.

Amesema Baraza la Wawakilishi litavunjwa mara baada ya kukamilika kwa Mkutano wa 19 wa Baraza la 10, ambapo miongoni mwa shughuli zake kuu ni kupitisha bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Raya amesema baada ya kukamilika kwa shughuli za bajeti, Kiongozi wa Shughuli za Serikali ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdullah, alilihutubia baraza, hatua ambayo inaashiria kufungwa rasmi kwa shughuli za mkutano huo na pia kuhitimisha maisha ya Baraza la 10. Baraza hilo liliitishwa kwa mara ya kwanza Novemba 8, 2020, na kuzinduliwa rasmi na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi Novemba 11, 2020.

Aidha, amesema kumalizika kwa uhai wa baraza hilo kunatokana na masharti ya Kifungu cha 92(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachobainisha kuwa maisha ya baraza yataendelea kwa muda wa miaka mitano tangu kuundwa kwake.

Baraza hilo lilikuwa na jumla ya wajumbe 77, wakiwemo wajumbe 50 waliopatikana kwa kuchaguliwa majimboni, saba walioteuliwa na Rais, 18 wa viti maalum, mmoja akiwa Spika wa Baraza na mmoja Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kati ya wajumbe wote 77, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa na wajumbe 70, ACT-Wazalendo sita, na mmoja kutoka chama cha ADA-TADEA.