Wakati mazungumzo ya kidiplomasia yakiendelea mjini Geneva, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanakutana New York, kujadili mzozo kati ya Israel na Iran.
Akitoa hotuba yake ya ufunguzi kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres ameonya kuwa kutokana na kuendelea kwa mzozo kati ya Israel na Iran, dunia "inaelekea kwa kasi" kwenye mgogoro.
"Kuongezeka kwa mzozo huu kunaweza kuwasha moto ambao hakuna anayeweza kuudhibiti," amesema.
Guterres ameongeza kuwa anaamini kiini cha mzozo huo ni "suala la nyuklia."
"Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia. Lakini tutambue kuna pengo la kuaminiana," amesema.
"Ninatoa wito wa kukomesha mapigano na kurejea kwenye mazungumzo mazito."
Wakati UN ikitoa tahadhari hiyo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ulaya leo Juni 20, 2025, wamekutana na mwenzao wa Iran, Abbas Araghchi, mjini Geneva katika jitihada za dharura za kutuliza mzozo huo wa Mashariki ya Kati.
Mkutano huu, ikiwa utakwenda kama ilivyopangwa, utakuwa mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana kati ya Tehran na serikali za Magharibi tangu Israel ilipoishambulia Iran wiki moja na nusu iliyopita, na unaashiria ushiriki muhimu zaidi wa Ulaya katika mzozo huo, unaotishia pamoja na mambo mengine, biashara ya kimataifa.
Wakati huo huo, Rais Donald Trump, wa Marekani anayeiunga mkono Israel amesema bado anataka kutoa fursa kwa mazungumzo, jambo linalotoa nafasi kwa diplomasia kabla ya uwezekano wa hatua za kijeshi za moja kwa moja za Marekani.
Kabla ya mzozo huu kuzuka, Marekani ilikuwa ikifanya mazungumzo yake ya pande mbili na Iran kwa ajili ya mkataba mpya wa nyuklia, ikiiweka kando Ulaya ambayo ilikuwa na jukumu muhimu katika makubaliano ya mwaka 2015 ambayo Rais Trump aliyajiondoa katika muhula wake wa kwanza. Hali hii inaifanya Ulaya sasa ijaribu kurejesha nafasi yake kama mpatanishi mkuu.
Mawaziri wa Ulaya, wakiwemo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, wanatarajiwa kumsihi Iran kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Iran imeeleza nia yake ya kufanya hivyo, lakini imesisitiza kuwa haitafanya mazungumzo ikiwa chini ya mashambulizi.
Kabla ya mkutano huo muhimu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, ametoa matumaini akisema: "Kuna fursa sasa ndani ya wiki mbili zijazo kufikia suluhisho la kidiplomasia." Kauli hii inakuja baada ya Ikulu ya White House kusema Donald Trump atatoa uamuzi wake ndani ya wiki mbili zijazo kuhusu kuchukua hatua za moja kwa moja za Marekani.
Hadi sasa, hali ya mapigano inaendelea kati ya Israel na Iran. Jeshi la Israel limesema limewashambulia malengo kadhaa ikiwemo kile lilichokiita maeneo ya kutengeneza makombora jijini Tehran, huku upande wa Iran ukiendelea kujibu mashambulizi na hakuna upande unaoonekana kurudi nyuma.
BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED