Katika Mahakama ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Neema Christopher, imefunguliwa shauri la jinai namba 14859/2025, Jamhuri dhidi ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Lualaje Matatizo Kubelo Mwambipile.
Mshtakiwa anashtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa chini ya kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Mshtakiwa alikuwa ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya katika nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Lualaje kilichocho Kata ya Lualaje
Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Kissa Ngoloke, Juni 18, 2025 alisema mshtakiwa aliomba na kupokea rushwa ya kiasi cha sh. 800,000/= ili aweze kumsaidia mwanakijiji mmoja kumpatia sehemu ya shamba la kijiji, hivyo kuisababishia hasara halmashauri hiyo kiasi cha Sh. 800,000/-.
Mshtakiwa amekubali kutenda kosa hilo na kutiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini ya sh. laki tano (500,000) au kutumikia kifungo cha miaka 3 jela.
Pia ameamriwa kurejesha sh. laki nane (800,000) aliyopokea kwa njia za rushwa.
Mshtakiwa amelipa faini ya sh. laki tano(500,000) na amerejesha sh. laki nane (800,000/=).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED