Vyama vya msingi vya mkoa wa Pwani vinavyosimamia ukusanyaji wa zao la ufuta vimetakiwa kuorodhesha kwa usahihi majina ya wakulima ili kuhakikisha wanalipwa fedha zao kwa wakati pindi mauzo ya ufuta yanapofanyika.
Mbali na kuwataka kuorodhesha kwa usahihi majina ya wakulima, viongozi wa vyama hivyo pia wametakiwa kuweka bei za mauzo kwenye mbao za matangazo ili wakulima waweze kujua mapato yao yatokanayo na wanunuzi waliouziwa ufuta kupitia mnada.
Hayo yamesemwa na Meneja wa CORRECU Mkoa wa Pwani, Hamis Mantawela, alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari katika mnada wa pili wa ufuta uliofanyika kwenye ghala kuu la Kingoma, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
“Tunataka kila kiongozi wa chama cha msingi kuhakikisha anaorodhesha kwa makini majina ya wakulima ili waweze kulipwa pesa zao kwa wakati na kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza,” alisema Mantawela.
Aidha, aliwataka viongozi wa vyama hivyo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na si kwa upendeleo au kufanya udanganyifu kwa kupiga simu kuingiza taarifa hewa kabla ya kupokea mzigo.
“Viongozi wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata taratibu rasmi, si kwa matakwa yao binafsi,” aliongeza.
Mantawela pia alionya dhidi ya matumizi ya mazingira ya kubeti katika biashara ya ufuta, akisema yapo maghala yanayosomeka kuwa na tani 200 za ufuta, lakini baadaye inagundulika mzigo halisi ni tani 100 tu.
Vilevile alisisitiza kuwa wasafirishaji hawapaswi kuchukua magari yao na kupakia ufuta bila kupata oda rasmi kutoka kwa wakuu wa maghala.
Kwa mujibu wa Mantawela, zaidi ya shilingi bilioni 10 zinatarajiwa kulipwa kwa wakulima wa ufuta kupitia mnada wa kwanza uliofanyika Kibiti, mkoani Pwani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CORRECU Mkoa wa Pwani, Mussa Mng’reza, alisema serikali imeweka utaratibu wa kuuza ufuta kwa njia ya mnada ili wakulima waweze kuona moja kwa moja jinsi wanunuzi wanavyonunua mazao yao.
Mng’reza alisisitiza kuwa viongozi wa maghala wanapaswa kusimamia kwa weledi biashara hiyo ili kuhakikisha mkulima ananufaika ipasavyo.
Alisema malipo lazima yatolewe kwa wakati na akaonya waendesha maghala dhidi ya tabia ya kuhujumu utaratibu wa kuingiza ufuta kwenye maghala.
“Waendesha maghala mmeanza tabia isiyo sahihi ya kufanya hujuma katika maghala. Kuna maghala unakuta yana orodha ndogo ya ufuta, lakini baada ya muda unakuta mzigo umeongezeka ghafla,” alisema.
Aidha, aliwasihi wakulima kuhakikisha wanapeleka ufuta bora ili wanunuzi waweze kuununua bila shida yoyote.
Mng’reza alisema katika mnada wa kwanza ufuta uliuzwa kwa bei ya zaidi ya shilingi 2,000 kwa kilo, na mnada wa pili kumekuwa na ongezeko la bei ya kuuzwa kwa zao hilo. Alifafanua kuwa mnada wa kwanza ulikusanya zaidi ya kilo milioni tatu za ufuta, huku mnada wa pili ukikusanya zaidi ya kilo milioni nne.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Korombo, akizindua mnada wa kwanza wa ufuta uliofanyika Kibiti, aliwataka wakulima kusimamia ubora wa ufuta wanaoupeleka sokoni.
Alihimiza usafirishaji wa mizigo kufanyika kwa wakati na kila mkulima kuhakikisha mzigo wake unafika katika ghala kuu, huku akisema serikali itaendelea kuwasaidia wakulima kuinuka kiuchumi.
“Tunaishukuru serikali kwa kuweka utaratibu mzuri kwa wakulima kuuza mazao yao kupitia minada rasmi badala ya kuuza kwa kutumia vibakuli,” alisema Kanali Korombo.
Aidha, alionya dhidi ya utoroshaji wa mazao kwa kuwa kitendo hicho kinasababisha upungufu wa mazao sokoni na pia kupunguza takwimu rasmi za mkoa.
“Utoroshaji wa mazao unachangia hata kupunguza takwimu za mkoa wetu,” alisisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED