Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Senga Gugu, amefungua Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, chenye hadhi ya Daraja B, ambacho kimejengwa kwa thamani ya shilingi milioni 798.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa kituo hicho, Katibu Mkuu Gugu amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake kubwa za kuboresha sekta ya usalama nchini.
Pia amemshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa, kwa mchango wake mkubwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho.
Katibu Mkuu Gugu amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali imejitahidi kuhakikisha inaboresha miundombinu ya vituo vya Polisi, likiwemo Kituo hicho cha Daraja B kilichojengwa kwa mfumo wa kutumia mafundi wa kawaida.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni matokeo ya jitihada za Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, kupitia nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za kiusalama, kudhibiti uhalifu na kulinda raia pamoja na mali zao.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, ameishukuru serikali pamoja na Jeshi la Polisi chini ya IGP Camillus Wambura kwa kutambua umuhimu wa kuboresha miundombinu ya vituo vya Polisi, kutoa vitendea kazi, na kupandisha vyeo kwa askari.
Amesema hatua hizo zimekuwa chachu ya kuongeza morali kwa askari Polisi nchini na kuchochea uwajibikaji na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED