Rais Samia chifu Hangaya awa mtemi wa Sungusungu mikoa mitano

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:45 PM Jun 21 2025
RAIS Samia Suluhu Hassan
PICHA: MPIGAPICHA WETU
RAIS Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan amepewa heshima na hadhi ya kuwa Mtemi wa Sungusungu, jeshi la jadi, kwa mikoa mitano ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Tabora.

Rais  Samia ambaye pia ni Mwenyekiti CCM Mkuu akijulikana kwa jina la Chifu Hangaya, ametangazwa rasmi kuwa Mtemi wa Sungusungu kupitia risala ya utii wao kwake, wakati wa hafla ya kumpongeza kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati, iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, mkoani Mwanza, leo Juni 20, 2025.

“Mheshimiwa Rais (Dkt. Samia) kwa kuwa wewe ni Amiri Jeshi Mkuu, na sisi ni walinzi wako, watiifu kabisa, tunaomba upokee hadhi ya kuwa Mtemi wa Sungusungu. Nakukabidhi vifaa vya ulinzi wa jadi, ambavyo vitatolewa maelezo. Aidha, tunaomba tukutambulishe watemi na makamanda wa Sungusungu, ambao tumekuwa tukishirikiana katika mikoa hii mitano,” amesema Ndugu Richard Bundala, kiongozi wa Sungusungu hao.

Mtemi wa Sungusungu Kanda ya Ziwa, Sumbe Martine Mogani amemkabidhi  Samia silaha za kijadi, ambazo ni upinde na mishale, pamoja na mavazi ya kaniki na kofia, ikiwa ni ishara ya kumpatia heshima na hadhi hiyo ya kuwa mtemi wa Sungusungu katika mikoa hiyo mitano.

Kwa upande wake,  Rais Samia amewapongeza Sungusungu kwa kutimiza miaka 42 tangu jeshi hilo la ulinzi wa jadi lilipoanzishwa kwa nia ya kuitikia wito wa kisera wa ulinzi na usalama, uliomtaka kila Mtanzania kuwa mlinzi ndani ya nchi yake, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na mamlaka za kisheria, hasa Jeshi la Polisi, kupitia polisi jamii, katika kulinda amani na utulivu wa nchi katika maeneo yao.

Rais Samia pia amewapongeza walinzi hao wa jadi kwa mchango mkubwa ndani ya muda huo wote tangu kuanzishwa kwao, huku akiwataka kuendelea kuwa sehemu ya ulinzi na usalama wa mali na miradi ya maendeleo ambayo nchi imeanzishwa na kukamilishwa kwa gharama kubwa kote nchini.