Wasanii mahiri wa muziki wa Bongo Fleva, Chege Chigunda na Madee, maarufu kama ‘Samia Kings’, wamenogesha Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), Sabasaba, kwa kuhamasisha watanzania kuenzi na kununua bidhaa zenye nembo ya ‘Chapa Tanzania’ (Made in Tanzania).
Wasanii hao walipokelewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dk. Kedmon Mapana, katika banda la Karume ambalo linaonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na watanzania.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Madee amesema ambao hawajafika katika maonesho hayo wafanye hima, ili kushuhudia bidhaa zinazotengenezwa na wazawa.
“Kama bado hujafika kwenye banda letu la ‘Made in Tanzania’, umepata dhambi. Kuna vitu vingi sana vya asili yetu ambavyo huwezi kuviona popote. Hii ni fursa ya kipekee kujifunza na kujivunia vyetu.”
Ameongeza kwa kusimulia kisa alichokutana nacho nje ya nchi aliponunua bidhaa zenye asili ya Afrika lakini zikiwa na nembo ya mataifa mengine:
“Nilinunua nyanya na vitunguu ambavyo nilijua kabisa vimetoka Tanzania, lakini ziliandikwa Made in nchi nyingine. Hii inaumiza. Ndiyo maana huu mpango wa Made in Tanzania ni ukombozi mkubwa kwa sisi waishio nje na wenye mapenzi na bidhaa za nyumbani.”
Kwa upande wake, Chege, amesisitiza kuwa Sabasaba inafanyika nyumbani kwake yaani Temeke, akijutia kutomleta binti yake Jada, kwenye maonesho hayo.
“Ningekuja naye tungenunua bidhaa nyingi za Kitanzania. Watoto wana mapema. Nawaomba wazazi wenzangu tuwalete watoto wetu, ndiyo kizazi cha kesho,” alisema.
Chege ameeleza kuvutiwa na ubunifu wa mavazi, viatu na bidhaa nyingine za viwandani vinavyotengenezwa hapa hapa nchini.
Msanii kutoka Afrika Kusini, amesema amevutiwa na ubora wa bidhaa za Tanzania na kuahidi kuwa balozi wa kuzitangaza kwa wenzake nyumbani..
Dk. Mapana, amewahimiza watanzania kutumia fursa ya Sabasaba kutembelea banda la Karume kujionea ubunifu wa ndani na kushiriki kukuza uchumi wa nchi kupitia bidhaa za ndani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED