CCM, CPC China wajadili ushirikiano zaidi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:14 PM Jul 12 2025
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Viongozi hao kutoka China katika kikao kilichofanyika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui
CCM
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Viongozi hao kutoka China katika kikao kilichofanyika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Dimwa, amesema Chama Cha Mapinduzi kinajivunia kuimarika kwa mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China.

Dk. Dimwa ameyasema hayo leo Julai 12,2025 wakati anazungumza na wageni kutoka China waliotembelea Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui kwa ajili ya  kujadili na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kimaendeleo baina ya CCM na CPC, amesema 

Katika mazungumzo hayo kwa pande zote mbili zilijadiliana namna ya kuendeleza uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria, uliojengwa juu ya misingi ya mshikamano wa vyama vya ukombozi, usawa na maendeleo ya pamoja. 

Dk. Dimwa ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na China ulianza kustawi baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kuimarika zaidi baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 

Amesema historia hiyo imejengwa juu ya misingi ya mshikamano wa kimapinduzi, alikumbusha namna China ilivyokuwa mshirika wa kweli wa Tanzania katika kipindi kigumu cha ukoloni, ukombozi na ujenzi wa taifa jipya. 

Kwa mujibu wa  Dk. Dimwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China ni mfano wa mafanikio ya sera ya kutoegemea upande wowote. 

Amesema China imekuwa mdau mkubwa katika kulinda uhuru na kujitegemea kwa Tanzania, sambamba na kuunga mkono sera zake za kijamaa. 

Dk. Dimwa amesema ushirikiano kati ya China na Tanzania haujaishia katika diplomasia tu, bali umeenea katika maeneo mengine muhimu ya kipaumbele kama ulinzi na usalama, afya, elimu, miundombinu, utalii, kilimo, michezo na biashara. 

Aidha, amepongeza juhudi za serikali ya China, kupitia Chama cha CPC kusaidia miradi ya maendeleo, hasa katika kujenga hospitali, barabara, na vituo vya afya, sambamba na kutoa nafasi za masomo na mafunzo kwa vijana wa Kitanzania wa fani mbalimbali za kipaumbe. 

Kuhusu ushirikiano wa kisiasa, Dk. Dimwa amesema kuwa uhusiano wa kihistoria kati ya CPC na CCM unaendelezwa kwa mafunzo ya viongozi, kubadilishana uzoefu wa uongozi na kushauriana juu ya sera za maendeleo. 

“Vyama hivi viwili vinashirikiana katika kusimamia ajenda za kisiasa zinazolenga ustawi wa wananchi na kuhimiza maadili ya uzalendo, mshikamano na maendeleo jumuishi,”amesema Dk.Dimwa. 

Kuhusu hali ya kisiasa ya ndani, Dk. Dimwa amesema CCM inaendelea na mchakato wa uchaguzi wa ndani kwa ajili ya kupata wagombea wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani watakaopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. 

Amesema chama hicho kimejipanga kwa ushindi mkubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya mwaka 2020/2025, na kwamba wanatarajia kuendeleza mafanikio hayo kupitia Ilani mpya ya 2025/2030, itakayozingatia mahitaji ya wananchi wote bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila. 

Dk. Dimwa ameishukuru CPC na Rais Xi Jinping kwa kuendeleza ushirikiano huo, na kutoa wito kwa China kuendelea kutoa mafunzo ya kiutendaji, nafasi za masomo, na ujenzi wa uwezo kwa watumishi wa umma, sekta binafsi, pamoja na viongozi na watendaji wa CCM na jumuiya zake. 

Kwa upande wake, Prof. Jiang Zuojun, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CPPCC na mkuu wa msafara wa China, alieleza kuwa lengo la ziara yao ni kujadili kwa kina namna ya kuendeleza mipango ya pamoja ya maendeleo baina ya China na Tanzania, kwa kuzingatia masuala ya sayansi, teknolojia, ubunifu, uongozi, matumizi bora ya rasilimali za bahari, uwekezaji na utalii. 

Amesisitiza kuwa China ina dhamira ya kuendelea kusaidia Tanzania katika sekta zenye kipaumbele kama kilimo cha kisasa, afya, elimu, miundombinu, na kuongeza fursa za masomo kwa vijana wa Kitanzania ili kuongeza wataalamu na maarifa katika nyanja muhimu za karne ya 21.