KOCHA wa Makipa wa timu ya vijana ya Yanga Masoud Slim amesema kuwa kikosi chao kinaendelea vema na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Safari Lager utakaochezwa Julai 26, mwaka huu kwenye uwanja wa KMC Mwenge Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 12 kwenye hafla ya kutambulisha kikosi cha wachezaji 22 wanaoiunda timu ya Safari Lager iliyofanyika kwenye viwanja vya Kunduchi (Dar es Salaam) amesema kwa upande wao wapo tayari kukutana na timu hiyo kwani kila mchezaji morali yake ipo juu.
"Kwa upande wetu tumejipanga vizuri kukutana na wapinzani wetu hao tunaipongeza safari kwa kuamua kuendesha kampeni hii yenye lengo la kuinua vipaji vya vijana kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania, amesema Slim.
Amesema huu ni mwaka wa pili kufanya hivyo na kudai kupitia kampeni hiyo wamefanikiwa kupeleka vijana wanne kwenda kucheza nje ya Tanzania.
Kocha huyo amewataka vijana kutumia vizuri vipaji vyao ili waweze kufika mbali zaidi na kuweza kutimiza malengo yao.
Kwa upande wake mchezaji wa timu ya vijana Komein Abubakari ambaye amezungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake amesema wapo tayari kukutana na wapinzani wao katika mchezo huo ambao utakuwa na upinzani mkubwa.
"Sisi kama wachezaji tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata matokeo katika mchezo huo kwa kufuata vizuri maelekezo ya benchi letu la ufundi.
Naye Meneja maudhui wa Klabu ya Yanga Abiudi Shayo (Priva) amewataka watanzania pamoja na mashabiki wa mpira wajitokeze siku hiyo kushuhudia vipaji vitakavyoonyeshwa na vijana hao.
Kikosi hicho kimepatikana kupitia kampeni ya kusaka vipaji iliyofanyika katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, pamoja na Dar es Salaam.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED