Dk. Mpango asisitiza ushiriki serikali, wadau wa afya na jamii kuimarisha huduma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:40 PM Jul 12 2025
Picha ya pamoja ya wadau na Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma
Picha: Mpigapicha Wetu
Picha ya pamoja ya wadau na Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa afya na jamii katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri unaofanyika jijini Dodoma.

Mkutano huo umeoongozwa na kauli mbinu “Wajibu wa Waganga Wakuu katika Kuimarisha Ubora wa Huduma za Afya kuelekea Bima ya Afya kwa Wote.” uliwashirikisha wadau mbalimbali walishiriki wakiwamo Amref Health Africa nchini Tanzania.

Dk.Mpango amesema serikali  itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wataalamu wa afya ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku akitambua mchango muhimu wa wadau wa afya katika kuleta ubunifu, kujenga uwezo na kufikia wananchi walioko pembezoni.

 Amebainisha kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kushirikiana na kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.


Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dk. Florence Temu, ameeleza kuwa ushiriki wa Amref Tanzania katika mkutano huu ni sehemu ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya afya ngazi ya jamii, mikoa na halmashauri.


“Mkutano huu ni jukwaa muhimu kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa huduma za afya, kujadili changamoto na mafanikio, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” amesema Dk Temu.


Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri umeanza Julai 11, 2025, na unatarajiwa kuhitimishwa Julai 14, 2025. 

Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya afya wakiwemo viongozi wa serikali, mashirika ya kiraia, washirika wa maendeleo na wataalamu wa afya, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati shirikishi katika kuboresha huduma za afya nchini.


Amref Tanzania imeahidi kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuimarisha na kuboresha afya ya umma nchini. Kupitia ushirikiano wa kimkakati, ubunifu, na mbinu zinazozingatia jamii, Amref itaendelea kufanya kazi kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote nchini Tanzania.