Ushirikiano NACTVET, China wazidi kung’ara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:47 AM Jul 12 2025
Ushirikiano NACTVET, China 
wazidi kung’ara
Picha: Mpigapicha Wetu
Ushirikiano NACTVET, China wazidi kung’ara

Tanzania na China zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi stadi (TVET) kwa faida ya pande zote.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Fredrick Salukele, katika ufunguzi wa semina ya  kubadilishana uzoefu na ujuzi  kati ya vyuo  vya TVET vya China na Tanzania, kwa niaba ya Waziri wa Elimu iliyofanyika Julai 11, 2025 katika ofisi za NACTVET, Kanda ya Mashariki Dar es Salaam. 

Dk. Salukele amebainisha kwamba mashirikiano yaliyopo ni dira ya pamoja na dhamira ya dhati ya kulijenga bara la Afrika kupitia elimu ujuzi na kwamba semina hiyo ni kielelezo cha nia njema  ya ushirikiano endelevu katika kukuza ujuzi, maarifa na ubunifu kwa maendeleo ya TVET nchini.

Alifahamisha kwamba  Semina ya nne mnamo mwaka 2024, iliwezesha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano na vyuo 10 kutoka China, ambapo pia wafanyakazi  12 wa NACTVET walishiriki ziara ya mafunzo nchini China kujielimisha juu ya  mifumo bora ya uendeshaji TVET.

Kwa upande wake, China imeahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo kubadilishana wataalamu, uandaaji  mitaala, uandishi wa vitabu vya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuanzisha programu za mafunzo zinazoendana na viwango vya kimataifa na mahitaji ya soko la ajira.
 
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTVET, Bernadetta Ndunguru amesisitiza kuwa Baraza litaendelea kuhakikisha kuwa mafunzo ya TVET yanayotolewa nchini yanakidhi ubora na mahitaji ya soko la ajira Kitaifa na Kimataifa.

Ujumbe wa China ukiongozwa na  Mkurugenzi  Mkuu wa Idara ya Elimu toka Sichuan, Prof. Yu Xiaoqi umebainisha kuwa, China itaendelea kushirikiana na Tanzania  katika sekta ya ellimu hususani TVET, ikiwa ni pamoja na uingizaji wa programu za Akili Unde au Mnemba (Ai), ili kuwezesha utoaji wa juu zaidi wa elimu ujuzi Tanzania.

Semina hiyo ni ya Tano kufanyika Tanzania ambapo wataalam kutoka vyuo vya TVET vya Tanzania na China wamefanya mawasilisho yenye shabaha ya kubadilishana uzoefu wa Kitaaluma katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET).