NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa jitihada zake katika kukuza sekta ya nyuki kupitia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zenye viwango vya ubora.
Pia, ametaka wakala huo kuongeza ubunifu zaidi katika vifungashio na taarifa za kitaalamu zitakazomsaidia mlaji kuelewa thamani ya bidhaa hizo. Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la TFS katika maonesho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Kitandula alisema kuwa bidhaa za nyuki, ikiwamo asali na nta, zina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na afya ya wananchi, na hivyo zinahitaji mikakati ya kuongeza ushindani sokoni.
“Ni jambo jema mmeweka korosho na asali pamoja, lakini mteja haelewi mchanganyiko huu unamnufaishaje kiafya, wala kiwango cha utafiti uliofanyika. Hili ni eneo muhimu la kuboresha. Toeni maelezo ya kina yanayomsaidia mlaji kufanya maamuzi sahihi,” alisema Kitandula.
Kitandula pia alisisitiza kuwa bidhaa hizo, ambazo hutengenezwa kwa kutumia rasilimali asilia, zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira na kipato kwa vijana na wanawake vijijini iwapo zitafungashwa na kutangazwa kwa weledi wa kibiashara.
Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka TFS, Emiliana Kiwango, alimweleza Naibu Waziri kuwa was wamejikita katika matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kutoa huduma na kusimamia biashara ya mazao ya misitu na nyuki, sambamba na mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha sekta ya umma kupitia teknolojia.
“TFS tumeweka kipaumbele katika matumizi ya teknolojia za kisasa, hasa mifumo ya kidijitali, katika utekelezaji wa majukumu yetu ya uhifadhi, uzalishaji na biashara ya mazao ya misitu na nyuki. Tunaendelea kuimarisha miundombinu ya utendaji kazi na kuifikia jamii kwa njia rafiki na bora zaidi,” alisema Kiwango.
Alisema TFS kupitia Idara yake ya Nyuki imekuwa ikihamasisha wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini, kujihusisha na ufugaji nyuki kwa lengo la kuongeza kipato, kuhifadhi mazingira, na kuongeza tija katika matumizi ya rasilimali za misitu kwa njia endelevu.
Maonesho ya wiki ya utumishi wa umma kwa mwaka 2025 yamebeba kaulimbiu isemayo “Utoaji wa Huduma Bora kwa Umma ni Msingi wa Maendeleo Endelevu”, yakiwa na lengo la kuhamasisha uwajibikaji, ubunifu na matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma.
Kwa mwaka huu, TFS inashiriki kwa kuonesha bidhaa za nyuki, huduma za kidijitali kama mfumo wa e-Misitu, pamoja na mafanikio ya uhifadhi wa misitu ya hifadhi za taifa, misitu ya asili, na programu za uwekezaji katika ekolojia endelevu ya misitu na nyuki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED