JOTO la kisiasa limezidi kupanda katika majimbo ya Mkoa Singida ambapo baadhi ya wabunge sasa wanatafuta wabaya wao kufuatia kuzimimina barua za kuwashitaki wanachama walioonesha nia ya kutaka kuingia kwenye kinyang'anyiro kupambana nao katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Barua hizo zilizoandikwa na baadhi ya wabunge hao wamezipeleka kwa viongozi wa ngazi ya mkoa na taifa, pia wanawalalamikia baadhi viongozi wa ndani ya chama waliopo katika majimbo yao kwa madai wanashirikiana na watia nia kuwahujumu.
Uchunguzi wa kina ambao umefanywa na Nipashe umebaini kuwa wabunge hao madai yao ni kwamba baadhi ya wanachama walioonesha nia kutaka kuwania kwenye majimbo yao wanafanya faulo nyingi kwa kuanza kampeni mapema.
Wabunge hao pia katika barua zao hizo ambazo gazeti hili imeziona wanawatupia lawama viongozi wa chama kwa maana ya watendaji wa ndani ya chama kwamba wameshindwa kuwadhibiti makada wanaotaka kutia nia ya kugombea ubunge.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa kinachifanywa na wabunge hao kumimina barua kila siku ni hofu tu iliyowajaa hasa kutokana na baadhi yao kutokuwa ba uhakika wa kurudi katika uchaguzi huu.
"Yaani kuna wabunge kila mara ni kuandika barua tu kushtaki wenzao kwa viongozi wa wa juu kwa tuhuma ambazo kimsingi hazipo sijui hofu yao ni ipi, watulio mchakato uanze na kama kuna mwanachama au mtia nia alikiuka utaratibu chama kipo macho," alisema kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM huku akimtaja mbunge mmoja ambaye ndiye anaongoza kwa kuandika barua kupeleka juu (jina tunalihifadhi).
Hadi sasa mchuano mkali upo katika jimbo la Singida mjini linaloongozwa na mbunge Musa Sima ambapo wanachama 15 wanadaiwa kujipanga kumkabili katika kinyang'anyiro hicho. Baadhi ya wanachama wanaotajwa kuingia kwenye kinyang’anyiro katika jimbo la Singida mjini ni pamoja na Mkurugenzi wa Kijiji cha Nyuki,Philemon Kiemi,Mkurugenzi wa Kiwanda cha Pamba, Sajjad Haider,Meya wa Manispaa ya Singida,Yagi Kiaratu na mkemia Japhar Said ambaye ni Mkaguzi Mwandamizi wa Dawa kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Wengine wanaotajwa kuingia katika kinyng’anyiro jimbo la Singida mjini ni Charles Kisuke, Juma Kilimba ambaye ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Singida, Hassan Mazala, Halima Sadi,Martin Lissu, Ibrahim Wawa.
Jimbo la Ilongero linaloongozwa na mbunge Ramadhani Ighondo ndilo linaonekana kuwa la moto zaidi katika majimbo yote ya mkoa huu kutokana na wanachama zaidi 20 kudaiwa kuwa wanajipanga kupambana na Ighondo.
Wanachama hao ni pamoja na Waziri mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu, mfanyabiashara maarufu anayemiliki viwanda vya kutengeneza magodoro, Haidary Gulamali na Maulid Sombi. Wengine wanaotajwa kutaka kumkabili Ighondo ni Alfred Ringi,Japhet Mungwe,Mercy Mumbee,Abdallah Haji,Chrisogone Mangi,Hashim Ntandu,Gloria Nkungu,Musa Kuji,Juma Sima,Rehema Majii,Amani Nyekele,Huruma Kilakuno,Baraka Mussa,Sabasaba Manase,Juma Ng'imba na Dk.Khalid Salla.
Jimbo la Singida Mashariki ambalo mbunge wake wa sasa ni Miraji Mtaturu nalo limetajwa kuwa la moto ambapo Thomas Mgonto ambaye ni mfanyakazi katika Bandari ya Dar es Salaam ametajwa kutaka kuingia katika jimbo hilo.
Mwingine ni Nusrat Hanje ambaye ni mbunge wa viti maalum Mkoa wa Singida kupitia Chadema ambaye ameshaweka wazi kwamba atagombea katika jimbo hilo kupitia CCM. Jimbo la Manyoni linaloongozwa sasa na Dk.Pius Chaya, Katibu Tawala Mkoa wa Singida mstaafu, Doroth Mwaluko anatajawa kulinyemelea na wengine wanaotajwa ni Jamali Kuigwa na mbunge mstaafu wa jumbo hilo Daniel Mtuka.
Katika jimbo la Iramba Mashariki ambalo mbunge wake ni Francis Mtinga naye anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida kupitia Chadema, Jesca Kishoa ambaye ameshatangaza kujitoa Chadema na sasa anapiga jalamba kugombea jimbo hilo kupitia CCM.
Wengine wanaotajwa kutaka kuingia katika kinyng’anyiro hicho ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega na kada mwingine aliyefahamika kwa jina la Baraka. Jimbo la Itigi linanyemelewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC), Yohana Msita ambaye tayari ameshaandika barua kujitoa kwa muda katika wadhifa wake huo ili aweze kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kumkabili vizuri mbunge wa sasa Yahaya Masare.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED