Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kaskazini, imeendesha mafunzo kwa wasambazaji na wauzaji wa gesi ya kupikia (LPG) katika Mkoa wa Manyara ili kuzingatia vigezo na masharti kwenye utoaji huduma.
Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Lorivii Long’idu, ameeleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa wadau hao kuhusu umuhimu wa kuzingatia vigezo na masharti katika utoaji wa huduma za usambazaji na uuzaji wa LPG ili kuepuka madhara na kufungiwa leseni. Pia amewataka wasambazaji wakuu nao kujenga tabia ya kuwapatia elimu wauzaji kuhusu masuala ya usalama.
Mhandisi Long’idu amesema EWURA inaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ukilenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Mhandisi wa Petroli, Magreth Mwita, ametoa utaratibu wa kupata leseni ya kusambaza na kuuza LPG, na kuwasisitiza kuzingatia matakwa ya kisheria na ya kiufundi katika biashara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na mizani na kuepuka uchakachuaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED