CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimependekeza magari yote ya serikali yatumie gesi asilia, kikisema hatua hiyo itaokoa Sh. bilioni 500.
Aidha, kimeshauri serikali iachane na matumizi ya 'mashangingi' na kutumia magari madogo, ili fedha za kununua na kuhudumia magari hayo, zielekezwe kwenye huduma za kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 21, 2025 kwenye mkutano wa uchambuzi wa bajeti kuu ya serikali 2025/26, Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita, amesema matumizi ya gesi asilia yatapunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta.
"Pendekezo hili pia litapelekea kupunguza matumizi ya Serikali kwa takribani Sh. bilioni 500 kwa mwaka. Hivyo basi, Bohari zote za Serikali (GPSA), zifungwe mitambo ya kujazia gesi asilia (CNG) mara moja," amesema Mchinjita.
Amewataka viongozi wa serikali kubana matumizi kwa kupunguza magari ya kifahari, posho, mishahara na safari za nje; na kuwachukulia hatua wabadhirifu wa mali za umma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED