Iran yafutilia mbali mazungumzo mapya ya nyuklia hadi mashambulizi yasitishwe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 AM Jun 21 2025
Wananchi Iran wakiandamana kuipinga Israel
PICHA: MTANDAO
Wananchi Iran wakiandamana kuipinga Israel

Iran imesema haitarejelea mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia huku ikishambuliwa, saa chache baada ya waziri wa ulinzi wa Israel kuonya kuhusu mgogoro wa "muda mrefu" na Jamhuri ya Kiislamu.

Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi alikutana na wanadiplomasia wa Ulaya mjini Geneva ambao walimtaka kufufua juhudi za kidiplomasia na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi yake.

Mwenzake wa Israel, Eyal Zamir, alisema katika hotuba yake ya video kwamba nchi yake inapaswa kuwa tayari kwa "kampeni ya muda mrefu" na kuonya "siku ngumu mbele".

Mapigano yalipamba moto usiku wa kuamkia leo huku jeshi la Israel likitangaza wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya hifadhi ya makombora ya Iran baada ya Iran kurusha makombora kuelekea Israel ya kati.

Milipuko ilisikika karibu na mji wa Tel Aviv nchini Israel. Ripoti zinasema kuwa jengo moja lilichomwa moto katikati mwa Israel kwa kuangukiwa na makombora. Araghchi alisema Iran iko tayari kuzingatia diplomasia mara tu "uchokozi wa Israel utakapositishwa".

Mpango wa nyuklia wa Iran ulikuwa wa amani, alisisitiza, na mashambulizi ya Israel yalikiuka sheria za kimataifa. Iran, aliongeza, itaendelea "kutumia haki yake halali ya kujilinda".

"Ninaweka wazi kwamba uwezo wa ulinzi wa Iran hauwezi kujadiliwa," alisema.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa aliishutumu Iran kwa kuwa na "ajenda ya mauaji ya kimbari" na kutoa tishio linaloendelea, akiongeza kuwa Israel haitaacha kulenga vituo vya nyuklia hadi "vivunjwe".

Rais wa Marekani Donald Trump alisema Iran ilikuwa na "kiwango cha juu" cha wiki mbili ili kuepuka uwezekano wa mashambulizi ya anga ya Marekani, akipendekeza kwamba anaweza kuchukua uamuzi kabla ya makataa ya siku 14 aliyoweka Alhamisi.

"Ninawapa muda, na ningesema wiki mbili zingekuwa za juu zaidi," Trump aliwaambia waandishi wa habari. Lengo, alisema, lilikuwa "kuona ikiwa watu wanapata fahamu zao au la". 


CHANZO: BBC