Kwimba yashika namba moja 'Mock' Kanda ya Ziwa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:52 PM Jun 04 2025
Kwimba yashika namba moja 'Mock' Kanda ya Ziwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Kwimba yashika namba moja 'Mock' Kanda ya Ziwa

Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imeibuka ya kwanza kati ya Halmashauri 43 ya mikoa sita ya Kanda ya Ziwa katika Mtihani wa Utimilifu wa darasa la saba ‘Mock’ Kanda.

Akizungumzia ufahulu huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Dk. Amon Mkoga amesema motisha, matumizi ya zana za kujifunzia pamoja na ushirikiano ya wanafunzi, walimu na maofisa ndiyo chachu ya kufikia hatua hiyo.

Dk.Mkoga amesema licha ya ufauli huo vilevile Wilaya hiyo imefanya vizuri katika masomo yaliyotajwa kushindikana ya Hisabati, Kiingerea na Sayansi huku malengo yao yakiwa ni kuwa miongoni mwa shule Halmashauri kumi bora katika mtihani wa Taifa.

Ofisa Elimu Taaluma Msingi wilayani humo, Simburya Simburya amesema katika mtihani huo uliohusisha mikoa ya Mara,Simiyu, Shinyanga, Kagera, Geita na Mwanza wao wameibuka namba moja kwa Halmashauri zote.

Amesema mikoa hiyo ina Halmashauri 43 na Shule 4,889 na kuwa matokeo yanaonesha kuwa baadhi ya masomo hayajafanywa vizuri likiwemo la Kiingereza, Hisabati pamoja na Sayansi lakini wao wameyafaulu.

“Hisabati tumekuwa wakwanza kwa ufaulu wa asilimia 96.64, Kiingereza wakwanza kwa asilimia 95.73 pia na somo la Sayansi na Teknolojia tumekuwa wakwanza kwa ufaulu wa asilimia 93.87,”alisema Simburya.

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Ng’wilabuzu Ludigija aliwapongeza walimu pamoja na maofisa elimu kata na Wilaya kwa kuhakikisha wanabadilisha taswira ya Wilaya hiyo na kuipa jina jipya.

“Tulizoea kila jambo baya tunapewa sisi, mara mimba na ndoa za utotoni tunaongoza mambo kama hayo yasiyo faa lakini ninyi mmejutahidi sasa na sisi tunaonekana katika mambo mazuri na msimamo wetu katika elimu,”alisema Ludigija.

Aidha aliwataka maofisa elimu kuendelea kuandaa utaratibu wa kutoa motisha kwa shule na walimu wanaofanya vema ili kuwapa moyo wa kuendeleza juhudi katika kazi yao.