Moto wazua taharuki Chuo cha MUST, bweni la wasichana lateketea

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 06:17 PM May 20 2025
Moto wazua taharuki Chuo cha MUST, bweni la wasichana lateketea

Taharuki imetanda katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) baada ya moto mkubwa kuliteketeza moja ya mabweni ya wasichana, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali pamoja na kujeruhi mwanafunzi mmoja.

Tukio hilo limetokea mapema leo Mei 20, asubuhi, wakati wanafunzi wengi wakiwa darasani. Inadaiwa kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyosababishwa na matumizi ya jiko la umeme (heater), kifaa ambacho hakiruhusiwi kutumika chuoni hapo.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Malumbo Ngata, amesema moto huo ulianzia katika chumba kimoja cha bweni ambacho kilikuwa na wanafunzi wanane.

“Mwanafunzi aliyekuwa chumbani wakati moto ulipozuka amejeruhiwa kwa kiasi kidogo. Tunamshukuru Mungu kwa kuwa wanafunzi wengine walikuwa tayari wapo madarasani, hivyo waliepuka madhara makubwa,” amesema Kamanda Ngata.

Ameongeza kuwa mali zote zilizokuwemo ndani ya chumba hicho, ikiwemo kompyuta mpakato, vitabu, na nguo, zimeteketea kabisa.

Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Dk. John John, amesema chuo kimetangaza kuunda kamati maalum kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo na kufanya tathmini ya hasara iliyojitokeza kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Tumechukua hatua za awali za kuwahamisha wanafunzi wote waliokuwa kwenye bweni hilo na kuwapeleka kwenye bweni jipya kwa usalama wao. Tunaomba muendelee kuwa watulivu wakati jambo hili linashughulikiwa,” amesema Dk. John.

Amesema kuwa kwa wanafunzi waliokuwa na mitihani, idadi ya masomo na ratiba mpya itaandaliwa na Idara ya Taaluma ili kuepusha athari za kielimu.

Uongozi wa chuo umesisitiza kuwa taarifa rasmi ya uchunguzi na hatua zaidi itatolewa mara tathmini kamili itakapokamilika ili kuondoa sintofahamu kwa wanafunzi na jumuiya nzima ya chuo.