Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wataendeleza amani na utulivu ili wananchi wafanye shughuli zao za maendeleo, na kutaka wale wenye hila na mipango ya uchochezi na kutaka kuwagawa watu wasipewe nafasi.
Amesema Rais Samia ni mzalendo na mwadilifu ambaye kwa utajiri wa rasilimali za nchi anazisimamia ndio maana miradi mbalimbali inatekelezwa.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, CPA Amos Makalla, ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Katoro, mkoani Geita, katika mkutano wa hadhara wakati akiendelea na ziara yake ya siku saba ikihusisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza na Simiyu.
“Kama kuna Mtanzania anabeza maendeleo tuliyopata kama kuna gari la wagonjwa akimbizwe Hospitali ya Milembe.Yamefanyika mengi tunakushukuru, ili tuendelee kupata maendeleo tudumishe amani,” amewataka Watanzania.
Amewaeleza Katoro na Busanda na Watanzania kwa ujumla kuwa Chama Cha Mapinduzi ndicho chenye amani.
Makalla amesema kwa ushindi ambao wamekipa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji kwao ni deni kubwa, kitaendelea kuwa karibu na wananchi kutatua kero zao na kuwaletea maendeleo.
“Wachimbaji wadogo amesema hapa Mjumbe Halmashsuri Kuu Taifa, azma ya serikali ni kujali wachimbaji wadogo, wameendelea kuunga mkono jitihada za kuwajali wachimbaji wadogo.
“Azma ya chama ni kuhakikisha tunawajali wachimbaji wadogo, hao wakubwa walianza kama wadogo, wakipewa fursa wadogo watakua, hivyo azma ya CCM ni kuwajali wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa,” amesema.
Makalla amesema Mkoa wa Geita una madini na kwamba wana Rais Samia ni mzalendo na mwadilifu ambaye kwa utajiri wa rasilimali za nchi anazisimamia ndio maana miradi mbalimbali inatekelezwa.
“Hapa wanaleta mradi wa maji wa Sh. bilioni sita, barabara, huduma za afya,” amesema.
Makalla amesema walikwenda hapo na kukuta shida kubwa ya maji ambapo chini ya Rais Samia kero inakwenda kuisha,” amesema.
Amesema pia, zimepelekwa Sh. milioni 800 kuongeza usambazaji huduma hiyo kwa wananchi.
“Ilikuwa ukipita hapa usiku ni giza, lakini Rais Samia ameleta fedha kuwawekea taa 170 katika mji wenu, kuna hospitali, barabara, tunaamini kwamba, miradi ya maendeleo imekuwa sehemu ya kushawishi wananchi kukiamini CCM,” amesema.
Mkuu wa Mkoa Geita, Martin Shigella, amesema Oktoba 15, mwaka 2022, Rais Samia alipita Katoro, ambapo barabara ilikuwa giza, lakini alichoahidi amekitekeleza na kufungwa taa barabarani ambazo zinawezesha wafanyabiashara kufanya biashara hadi siku.
“Barabara za lami kilometa mbili tumeanza na tunataka kuongeza hadi kilometa tano, wananchi wa Katoro waliomba halmashauri, tumepewa jimbo kwanza na tunaelekea kwenye halmashauri, tunaomba baada ya uchaguzi kazi hiyo uifanye kazi Mheshimiwa mgeni rasmi,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED