Mpasauko ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umechukua sura mpya visiwani Zanzibar, baada ya wanachama zaidi ya 200 wakiwemo viongozi 28, kutangaza kujivua uanachama, wakilalamikia kile walichokiita ukandamizaji na upotevu wa mwelekeo ndani ya chama hicho.
Uamuzi huo umetangazwa leo jioni, mbele ya waandishi wa habari na Atafat Hamad Ali, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) Wilaya ya Magharibi B, ambaye pia alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu la chama.
"Tumeamua kujivua uanachama kutokana na ukandamizaji mkubwa, ubaguzi na kukosekana kwa mwelekeo ndani ya chama. CHADEMA kimepoteza dira, na hatuoni tena sababu ya kuendelea kuwa sehemu ya chama hiki," amesema Atafat.
Kwa upande wake, Muslim Khamis Rajab, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mjini Magharibi, amesema wamechukua hatua hiyo kwa sababu chama kimeshindwa kutimiza matarajio ya Watanzania waliokuwa wakiamini katika harakati za mabadiliko.
"Ndoto za Watanzania zimekwama kutokana na siasa chafu na uongozi usiojali misingi ya demokrasia. Tumepoteza imani na mwelekeo wa chama hiki," amesema Muslim.
Hata hivyo, licha ya kutangaza kujiondoa CHADEMA, viongozi na wanachama hao hawakubainisha chama kingine cha siasa ambacho watajiunga nacho baada ya kujivua uanachama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED