Wakili maarufu na mwanaharakati wa haki za binadamu, Peter Madeleka, amejiunga rasmi na chama cha ACT-Wazalendo katika hafla iliyofanyika mapema leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita, amesema kuwa Madeleka ni mmoja wa wanaharakati waliokuwa wakipigania haki kwa misingi ya usawa na kutokuwa na upendeleo wowote.
“Kumkaribisha Madeleka katika chama chetu ni ishara kuwa ACT-Wazalendo iko tayari kuwapokea wapambanaji wote wa haki, ili kwa pamoja tuweze kuendesha gurudumu la haki na usawa ndani ya chama na taifa kwa ujumla,” amesema Mchinjita.
Kwa upande wake, Wakiki Peter Madeleka amesema kuwa demokrasia ya vyama vingi nchini ilianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo na kuimarisha uchumi kupitia ushindani wa kisiasa.
“Nimejiunga na chama hiki ili kuchochea maendeleo ndani ya ACT-Wazalendo na kupambana na chama tawala, CCM, kwa lengo la kukiondoa madarakani kupitia sanduku la kura,” alisema Madeleka.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa Watanzania kushiriki kikamilifu katika chaguzi na kudai haki yao ya kupiga kura. “Tutahakikisha haki ya Mtanzania inapatikana kupitia uchaguzi. Endapo kutatokea mazingira yasiyotarajiwa, tutatafuta namna bora ya kukabiliana nayo lakini kwa msingi wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi,” aliongeza.
Hatua hii ya Madeleka inatafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama hatua muhimu kwa ACT-Wazalendo kuelekea uchaguzi mkuu ujao, ikionyesha wazi chama hicho kinavyoendelea kujijenga kwa kuvutia wanaharakati na viongozi wenye ushawishi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED